Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninaishi bila utaifa kwa zaidi ya miongo 7 sasa: Sergio Chakaloff 

Ukosefu wa uaifa ni changamoto inayowakumba watu wengi.
© UNDP/Mirfozil Khasanov
Ukosefu wa uaifa ni changamoto inayowakumba watu wengi.

Ninaishi bila utaifa kwa zaidi ya miongo 7 sasa: Sergio Chakaloff 

Haki za binadamu

Kutana na Sergio Chekaloff ambaye kwa zaidi ya miongo saba anaishi bila utaifa baada ya nchi tatu alizodhani kuwa ni asili yake ambazo ni Ujerumani, Urusi na Armenia zote kukataa kumtambua na  sasa kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR anaishi Ibiza nchini Hispania baada ya kupewa hadhi ya kutokuwa na utaifa. Kulikoni?

Ibiza nchini Hispania makazi mapya ya Sergio Chekaloff mwenye umri wa miaka 74 anayesema hana utaifa baada ya kuzaliwa kwenye kambi ya wakimbizi nchini Ujerumani mwaka 1946 walikokutana wazazi wake  ambako mama yake akifanyakazi ya utafsiri kwenye kambini hapo. 

“Mama yangu alikuwa Mjerumani, baba yangu Mrusi akitoka eneo la Yerevan ambalo sasa ni mji mkuu wa Armenia na alienda  kwenye vita vya pili vya dunia. Huko ndiko baba na mama yangu walikokutana kwenye kambi ya wakimbizi vita vilipomalizika na makambi kuundwa. Baada ya mwaka mmoja hivi nikazaliwa  na hapo walikuwa wanapanga kwenda Argentina” 

Sergio ameishi miongo sita Argentina akitumia kitambulisho cha kigeni kabla ya kuhamia Ibiza Hispania anakoishi sasa na familia yake akiwemo binti yake Tamara ambaye anasema,“Baada ya kujaribu njia zote na nilipotambua kwamba kulikuwa na tatizo ndipo tulipoanza kusaka suluhu” 

Kwa miaka mingi hadhi ya Sergio haikuorodheshwa popote hadi shirika la Umoja wa Mataifa la UNHCR lilipomsaidia kuomba hadhi ya kutokuwa na utaifa nchini Hispania ambayo aliipata rasmi mwaka 2019 kwa sababu kila alikodhani ni asili yake walimkana. “Kwa Waajentina wanasema mimi Mjerumani, kwa Wajerumani wanasema mi Mrusi, kwa Warusi wanasema baba yangu alizaliwa Armenia na Armenia hawajapata nyaraka yangu yoyote nao hawanitaki pia, hivyo sina utaifa.” 

Kwa mujibu wa UNHCR duniani kote kuna mamilioni ya watu wanaoishi kama Sergio Chekaloff bila utaifa wowote, ni hilo ni tatizo kubwa.