Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je umaskini watumbukiza watoto wa kike kutoa ngono kupata kitoweo?

Wavuvi wakijiandaa kuondoka kuelekea bahaini huko Yoff, Sengal.
Picha ya UN
Wavuvi wakijiandaa kuondoka kuelekea bahaini huko Yoff, Sengal.

Je umaskini watumbukiza watoto wa kike kutoa ngono kupata kitoweo?

Ukuaji wa Kiuchumi

Ukosefu wa usawa wa jinsia, ugumu wa kupata huduma na umaskini vinaripotiwa kuchochea kiwango kikubwa cha mimba za utotoni na na virusi vya Ukimwi VVU huko Homa Bay nchini Kenya. Taarifa hizo ni kwa mujibu wa ripoti mpya iliyoandaliwa na serikali ya kaunti ya Homa Bay kwa kushirikiana na wadau wake kupitia msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF. 

Huyu ni Ayesha, mtoto mwenye umri wa miaka 18 akiwa fukwe ya Sindo katika kaunti ya Homa Bay nchini Kenya.  

Simulizi yake ni miongoni mwa vyanzo vya ongezeko la maambukizi ya VVU kama ilivyoripotiwa katika ripoti mpya iliyoandaliwa kwa msaada wa UNICEF

Collins Ochieng Opiyo katibu wa mamlaka ya usimamizi wa fukwe ya Sindo anasema suala la wavuvi kubadilisha samaki kwa ngono ni jambo la siku nyingi na la kiuchumi na wanasaka kulitokomeza. 

Kwa Pierre Robert ambaye ni Mkuu wa kitengo cha VVU UNICEF nchini Kenya, kitendo cha mtu kukubali kutoa ngono ili apate kitoweo ni zaidi ya umaskini. “Nadhani uhusiano ulio nao na watu wanaokuzunguka, wanaoweza kukushawishi au kukushinikiza, ina dhima muhimu zaidi.” 

Ayesha akafunguka zaidi akisema, “Wengine wanasema nataka kulala na wewe nikuletee samaki, mwingine unaweza kulala naye na anataka kukupiga, hakupi fedha wala chochote, anasema mlikuja huku kutuibia fedha zetu na hawatupi.” 

Bwana Robert, anasema kitendo cha Ayesha na wengine kulazimika kuingia kwenye ngono ili wapate kitoweo ni ukatili wa kijinsia. “Kwa sababu pindi msichana anapokuwa hana chochote na anaona wenzake wa umri huu wanashiriki tabia hiyo, inarahisisha.” 

Kwa kutambua hatari ambazo watoto wa kike wanakumbwa nazo kwenye maeneo ya uvuvi huko Homa Bay, UNICEF imeliwezesha shirika la kiraia la LVCT kupatia watoto wa kike na wanaume elimu ya kinga dhidi ya VVU. 

Akifafanua msaada huo, Henry Ogallo Were, muuguzi kutoka shirika hilo anasema wanalenga wasichana wenye taarifa iwe shuleni au maeneo salama, na kuwapatia wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea mbinu za kujikinga na ujauzito, halikadhalika PEP ili kujikinga na VVU. 

Walengwa wengine ni wanaume kuanzia wavuvi, waendesha bodaboda na kwamba UNICEF imewezesha pia jukwaa la mtandao la kushirikisha vijana hasa kuwapatia msaada wa kisaikolojia wale wanaoishi na VVU.