Mume wangu na wanangu 4 waliuawa napata faraja kwa kuwasaidia wanawake wengine:Sabuni Chikunda

8 Disemba 2020

Tukiwa bado na siku 16 za harakati za kupinga uakatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, leo tunamulika mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC , Francoise Sabuni Chikunda ambaye amepitia madhila yasiyoelezeka, ikiwemo kubakwa na hata familia yake kuuawa, lakini yote hayo hayakumkatisha tamaa bali yamempa ujasiri wa kuwa nuru ya wanawake wakimbizi wenzake katika makazi ya wakimbizi ya Nakivale nchini Uganda.

Ni mwanaharakati Francoise Sabuni Chikunda akisema yeye mwenyewe ni mkimbizi lakini kwa sasa anawasaidia wanawake wenzake wakimbizi kuboresha maisha yao Nakivale Uganda. 

Anasema makazi ya Nakivale ni makubwa yakihifadhi wakimbizi wengi wakiwemo kutoka Congo, Rwanda, Burundi, Sudan, Eritrea na Ethiopia.  

Kazi na mchango mkubwa anaoufanya kuwasaidia wanawake umemwezesha kutambulika na hata kutwaa tuzo ya wakimbizi ya Nansen kwa kanda ya Afrika iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR mwezi Septemba mwaka huu wa 2020. Safari yake ilijaa mbigiri,“Nimepitia magumu mengi, mambo mengi sana. Nilipoteza nyumba yangu, familia yangu, kazi yangu na kila kitu. Nilibakwa mara nyingi, mume wangu na watoto wangu wanne waliuawa” 

Bi Chikunda ambaye alinusurika katika shambulio la mauaji ya kimbari ya 1994 na kukimbilia DRC, mwaka 2018 alitekwa na waasi lakini alifanikiwa kutoroka na kukimbilia Uganda kusaka usalama ambako hadi sasa anaishi kama mkimbizi anayewapa wanawake wenzie  matumaini,“Nawasaidia wanawake, kuwawezesha na kuwapa ujuzi, nawafundisha jinsi ya kujitegemea, nimewafundisha kutengeneza nywele, ufundi cherahani, kutengeneza maandazi , chapati na sambusa na pia natumia muda mwingine kuwapa ushauri nasaha wanawake na wasichana ambao walibakwa. 

Chikunda alianzisha  kikundi cha “Heri Yetu Foundation akiwa na wanawake 50, lakini kila siku idadi iliongezeka baada ya wanawake kuona mafanikio kwa wenzao na sasa kikundi hicho kina wanawake 1000 jambo linalompa faraja kubwa Sabuni Chikunda na kumsahaulisha japo kidogo machungu aliyopitia. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter