Tunaondoka DRC bila kuacha ombwe la usalama- MONUSCO

7 Disemba 2020

Harakati za kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa vikosi vya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO umekuwa ukiendelea sambamba na utekelezaji wa mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kuwa hatua hiyo haitaweka ombwe la usalama kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu.
 

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Leila Zerrougui amesema hayo wakati akiwasilisha mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ripoti kuhusu hali ya usalama na kibinadamu nchini humo.
Akihutubia kwa njia ya video kutoka Kinshasa, mji mkuu wa DRC, Bi. Zerrougui amesema mkakati huo wa pamoja unawakilisha dira ya pamoja ya upunguzaji taratibu wa vikosi, upunguzaji ambao wenye uwajibikaji na endelevu na hatimaye kufungwa kwa MONUSCO.

MONUSCO imeshaanza kufungasha virago

Bi, Zerrougui amesema, “mpito huu si mchakato ambao umeanza karibuni, bali ni mwendelezo wa hatua zilizochukuliwa kufuatia uchaguzi wa rais mwaka 2018 na kisha makabidhiano ya madaraka yaliyofanyika kwa amani. Tangu wakati huo, MONUSCO imeshafunga ofisi 9 za mashinani na hivi sasa tupo katika majimbo 6, pamoja na makao makuu ya ujumbe huo jijini Kinshasa.”

Hata hivyo amesema mkakati huo unatambua uhalisia nchini DRC na mahitaji ya kiusalama katika kila jimbo ambako MONUSCO bado ipo.

“Kwa hiyo basi mkakati huo unabeba mpango unaoendana na mazingira kulingana na jimbo husika, na unalenga kuimarisha uwepo wa MONUSCO katika amajimbo matatu yaliyoathiriwa zaidi na ghasia ambayo ni Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.,” amesema Bi. Zerrougui ambaye pia ni mkuu wa MONUSCO.

Amefafanua kuwa mujibu wa mkakati huo, ifikapo mwezi Juni mwaka 2021, MONUSCO itakuwa imeondoka kabisa Kasai na Juni 2022, iwapo kutakuwa na mafanikio na utulivu, basi itakuwa na uwezo wa kuondoka jimbo la Tanganyika.

 

Mashariki mwa DRC hali bado ni tete

Mkuu huyo wa MONUSCO amesisitiza kuwa bado hali ya usalama mashariki mwa DRC inatia wasiwasi mkubwa ambako kumeshuhudiwa mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na watu kufurushwa makwao.

Amesema “wakati shughuli za vikundi vilivyojihami bado zinashamiri huko Djugu na Irumu jimboni Ituri, ingawa kwa kiwango cha chini, bado mapigano ya kikabila na mashambulizi dhidi ya raia yameripotiwa huko Beni, Masisi na Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini na maeneo ya Uvira, Mwenga na Fizi jimboni Kivu Kusini.”

Umuhimu wa uwepo wa FIB

Amesisitiza kuwa shughuli za kikatili zinazofanywa na vikundi vilivyojihami va kigeni na vya nchini humo, zinaangazia umuhimu wa “kuendelea kwa shughuli za vikosi vya MONUSCO, ikiwemo kile cha kujibu mashambulizi, FIB ili kusaidia jeshi la serikali kukabili ghasia dhidi ya raia.”

Hata hivyo amekumbusha kuwa wajibu wa ulinzi wa raia unasalia mikononi mwa mamlaka za serikali, “na uendelevu wa kasi ya kipindi cha mpito cha MONUSCO unategemea uwezo wa serikali kubeba jukumu lake la usalama na kumarisha uwepo wa taasisi zake nchi nzima. Kwa sasa MONUSCO tayari inashiriki kikamilifu kusaidia serikali kutekeleza mpango wa marekebisho wa jeshi la polisi la taifa na marekebisho ya mfumo wa haki, kupitia makubaliano yaliyotiwa saini kati ya serikali na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP.”

Watu waliopoteza makazi yao katika ghasia Ituri DRC.
UNICEF/Madjiangar
Watu waliopoteza makazi yao katika ghasia Ituri DRC.

Mabadiliko na vikundi vipya vya MONUSCO

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mafunzo na utendaji wa kivita katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ ambao pia wanachangia walinda amani MONUSCO, “mabadiliko yaliyofanyika ni kupunguza baadhi ya askari kutoka vikosi vya awali na kuleta askari wapya na vikundi vipya vikiwemo vinavyoweza kufanya kazi kwa haraka zaidi yaani Quick reaction forces. Na hivyo vimeundwa na vikundi vitatu. Tanzania imeteuliwa  kuwa moja ya nchi ambazo zinaunda hivyo vikosi vya kuchukua hatua kwa haraka, na vikundi vinginevyo.”

Akihutubia kikao hicho kilichofanyika uso kwa uso ukumbini kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, mwakilishi wa kudumu wa DRC kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Paul Losoko Efambe Empole amesisistiza azma ya serikali yake ya kuvunja mzunguko wa mgogoro wa kivita nchini humo sambamba na ukosefu wa usalama mashariki mwa nchi.
Amesema wanataka kuona maisha ya kawaida yanarejea kwenye eneo hilo la DRC baada ya miongo miwili ya mzozo.
Hata hivyo amesema ili kufanikisha hilo “tunategemea msaada kutoka kwa wadau wetu wote wa DRC.”

Akisisitiza hoja hiyo, Bi. Zerrougui amesema  baadhi ya changamoto kubwa zinazokumba DRC kama vile uwepo wa vikundi vilivyojihami vya kigeni na vya ndani sambamba na usafirishaji haramu wa maliasili, zitahiaji jitihada za kikanda na kimataifa kuhakikisha zinapasiwa suluhu ya kudumu na endeleu.

COVID-19 na ulinzi wa amani

Mwakilishi huyo maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezungumzia pia changamoto ya janga la ugonjwa wa Corona, au COVID-19 katika kufanikisha wajibu wake wa ulinzi wa raia.
Amesema COVID-19 imekumba watendaji 173 wa MONUSCO ambapo 6 kati yao wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo.
Hata hivyo amesema wameweka mikakati ya kina kuzuia kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo sambamba na kuwapatia matibabu wagonjwa.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter