Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Udongo na bayoanuai ni lila na fila havitengamani: Bi. Mrema 

Mkulima  akiandaa shamba kwa kutumia jembe la kukokotwa kwa ng'ombe huko Bahir Dar Ethiopia.
Photo: FAO/Giulio Napolitano
Mkulima akiandaa shamba kwa kutumia jembe la kukokotwa kwa ng'ombe huko Bahir Dar Ethiopia.

Udongo na bayoanuai ni lila na fila havitengamani: Bi. Mrema 

Tabianchi na mazingira

Katika kuelekea siku ya udongo duniani itakayoadhimishwa kesho Jumamosi Desemba 5 Umoja wa Mataifa umesisitiza umuhimu wa kuhakikisha udongo una salia kuwa na rutuba na kulinda bayoanuai yake kwa ajili ya mustakbali wa uzalishaji wa chakula katika dunia hii na maisha ya binadamu. 

Katibu Mtendaji wa sekretarieti ya mkataba wa kimataifa kuhusu masuala ya Bayonuai (CBD) Elizabeth Mrema akisisitiza kuhusu hilo amesema,“Bayoanuai ya udongo ni muhimu sana ingawaje haitajwi au kutambulika mara nyingi. Inatoa huduma muhimu sana kwa mfumo wa maisha ya viumbe , ni muhimu kwa binadamu na afya ya mfumo wa viumbe vyote vilivyoko kwenye udongo kuanzia vile vidogo kama chembechembe hadi minyoo ya ardhini. Kila chembechembe ina jukumu muhimu katika mfumo wetu wa maisha , na tunavishukuru hivi viumbe kwa sababu ndio vinatupa udongo wenye rutuba kwa ajili ya chakula, maji safi tunayotumia na mfumo mzima wa uzalishaji. Hata hivyo pamoja na faida zote hizo udongo na viumbe vyake viko hatarini na katika tishio kubwa, tunahitaji kuchukua hatua kuvilinda na kuvitumikia.” 

Ameongeza kuwa bayoanuai inaendelea kupotea kila mahali na hatua zisipochukuliwa sasa basi maisha ya maliasili, mfumo mzima wa maisha na binadamu ikiwemo uhakika wa chakula vitakuwa njiapanda. Na kwa mantiki hiyo amesisitiza ,“Tunatakiwa kulinda bayoanuai ya udongo na kuchagiza masuala ya bayoanuai ya udongo kwa sababu yatatusaidia kutimiza lengo letu la kuishi kwa amani na maliasili. Tunahitaji kutambua haraka kwamba bayoanuai ya udongo haiwezi kutenganishwa na suala la uhakika wa chakula na ufikiaji wa malengo ya maendeleo endelevu , ni kama lila na fila . Bayoanuai ya udongo ndio muhimu, muhimili wa uzalishaji na mnepo wa kilimo kwa kuunda mifumo ya uzalishaji na ya maisha ili iwe na mnepo wa kuhimili dhidi ya majanga na changamoto zingine zitakazozuka.” 

Kaulimbiu ya siku ya udongo mwaka huu ni “Hakikisha uhai wa udongo, linda bayoanuai ya udongo” lengo likiwa ni kuelimisha kuhusu umuhimu wa kuhakikisha afya ya mfumo wa maisha na ustawi wa binadamu katika kushughulikia changamoto zinazoongezeka za udhibiti wa udongo, kupotea kwa bayoanuai, kuongeza uelewa wa udongo na kuzichagiza serikali, mashirika, jamii na watu binafsi kote duniani kuahidi kwa pamoja kuboresha afya ya udongo.