Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UN lataka hatua dhidi ya COVID-19 zinazojali watu na utu

Mkazi huyu wa akiwa eneo la soko la Konyokonyo mjini Juba nchini Sudan Kusini akivalia vizuri barakoa yake kujikinga na virusi vya Corona. UNICEF ilitengeneza barakoa 6,000 na kuzisambaza kwa wanajamii.
© UNICEF/Bullen Chol
Mkazi huyu wa akiwa eneo la soko la Konyokonyo mjini Juba nchini Sudan Kusini akivalia vizuri barakoa yake kujikinga na virusi vya Corona. UNICEF ilitengeneza barakoa 6,000 na kuzisambaza kwa wanajamii.

Baraza Kuu la UN lataka hatua dhidi ya COVID-19 zinazojali watu na utu

Afya

Janga la ugonjwa wa Corona, COVID-19 likiendelea kutikisa duniani, Umoja wa Mataifa hii leo umeanza kikao maalum cha ngazi ya juu cha siku mbili kujadili janga hilo ambalo hadi sasa limesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,400,000 duniani kote.

Lengo la kikao hicho ni kupanga mwelekeo ujao wa kimshikamano na unaojali zaidi watu na utu wakati huu ambapo kuna matumaini ya chanjo thabiti.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Volkan Bozkir amesema, "tumeitisha kikao hii ili kuweka njia ya pamoja ya kupunguza machungu ya watu tunaowahudumia. Huu si wakati wa kunyosheana vidole."

Kikao hicho kilianza kwa dakika moja ya kuwa kimya kukumbuka wale wote waliopoteza maisha wakiwemo wanafamilia na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Kama sehemu ya kampeni kuhusu COVID-19, kamanda wa Bangladesh anayehudumu katika MINUSCA nchini CAR akimhamasisha mkandarasi mwenyeji kuvaa barakoa.
MINUSCA
Kama sehemu ya kampeni kuhusu COVID-19, kamanda wa Bangladesh anayehudumu katika MINUSCA nchini CAR akimhamasisha mkandarasi mwenyeji kuvaa barakoa.

Kisha Katibu Mkuu Antonio Guterres akazungumza akisema "tangu mwanzoni, shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO) lilitupatia taarifa na miongozo ya kisayanasi na ya uhakika juu ya kile kinapaswa kuwa msingi wa hatua za pamoja za kimataifa dhidi ya COVID-19. Kwa bahati mbaya, mapendekezo mengi hayakufuatwa. Na pindi nchi zilipoamua kuchukua njia zao wenyewe, virusi vikaanza kusambaa kila upande."

Katibu Mkuu amesema wakati huu ambapo nchi wanachama zinasaka njia za kujikwamua, lazima kutumia fursa ya mabadiliko na kwamba, "chanjo haiwezi kuondoa uharibifu au shida zilizotokea ambazo zitakuwa nasi miaka kadhaa ijayo. Tunakabiliwa na mdororo wa kiuchumi kuwahi kutokea katika miongo minane . Ufukara nao unanyemelea, halikadhalika tishio la baa la njaa."

Mtengeneza kucha huko Ufaransa akiwa amejikinga vyema yeye na mteja wake dhidi ya COVID-19.
ILO/Marcel Crozet
Mtengeneza kucha huko Ufaransa akiwa amejikinga vyema yeye na mteja wake dhidi ya COVID-19.

Amesema changamoto hizi za vizazi na vizazi hazijasababishwa na COVID-19 pekee bali ni matokeo ya hali tete za muda mrefu, ukosefu wa usawa ulioshamiri sambamba na ukosefu wa haki, vitu ambavyo sasa vimewekwa wazi na janga la Corona na kwamba sasa ni lazima zifikie ukomo.

Kwa mujibu wa Guterres, kujikwamua kutoka athari za COVID-19 lazima kushughulikie hali zilizokuwepo hata kabla ya janga hilo, ikiwemo pengo katika huduma za afya hadi ongezeko la joto kupita kiasi katika sayari ya dunia.

"Mifumo thabiti ya afya na huduma za afya kwa wote (UHC) lazima view vipaumbele. COVID-19 ni janga la 6 kutangazwa na WHO kuwa janga la dharura na tishio la afya kwa umma tangu mwaka 2007 na halitakuwa la mwisho," amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema lazima kujifunza na kile kilichotokea iwapo viongozi wanataka kutimiza wajibu wao kwa watoto wao na wajukuu zao.

Kikao hicho cha siku mbili kitatoa fursa kwa viongozi wa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na viongozi wakuu wa Umoja huo na wadau wengine kubadilishana uzoefu wao katika harakati za kukabiliana na COVID-19, kutathmini vile nchi zimechukua hatua na kuweka hatua za pamoja za kukabili janga hilo, hatua ambazo zinajali utu na watu.