Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninaushukuru Umoja wa Mataifa kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma-Aneth Gerana Isaya 

Aneth Gerana Isaya,(katikati) mwanzilishi wa taasisi ya FUWAVITA nchini Tanzania inayowawezesha wanawake wenye ulemavu kupata stadi.
UN Tanzania
Aneth Gerana Isaya,(katikati) mwanzilishi wa taasisi ya FUWAVITA nchini Tanzania inayowawezesha wanawake wenye ulemavu kupata stadi.

Ninaushukuru Umoja wa Mataifa kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma-Aneth Gerana Isaya 

Haki za binadamu

Nchini Tanzania, taasisi ya FUWAVITA yaani Furaha ya Wanawake Viziwi Tanzania imekuwa ikiwawezesha wanawake wenye ulemavu nchini humo hususani wanawake viziwi kupata stadi za uongozi na ujasiriamali. Ahimidiwe Olotu wa Kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa amemhoji mwanzilishi wa taasisi hiyo, Aneth Gerana Isaya kupitia mkalimani wa lugha ya ishara Bwana Billbosco Muna. 

Aneth kupitia mkalimani wake huyo, akionea kwa lugha ya ishara, anasema, “sisi tumegundua kwamba wanawake wenye ulemavu ni kundi ambalo limesahaulika katika masuala mbalimbali kwa hivyo sisi tukaona tuweze kufanya harakati zetu kuhakikisha kwamba kundi hili linawezeshwa na kufikia zile ndoto zao.” 

Na kuhusu mafanikio ya wito na maono ya Umoja wa Mataifa kutaka asiwepo yeyote katika jamii anayeachwa nyuma kwa mazingira ya Tanzania, Aneth anasema, “binafsi nipende kuushukuru Umoja wa Mataifa kwa kuhakikisha wanaenda na kaulimbiu hii ya kuhakikisha kwamba hakuna mtu ambaye anaachwa nyuma. Kwa watu wenye ulemavu, sisi tunakumbanana changamoto nyingi zaidi kuliko wanawake wa kawaida. Kwanza kabisa ni kutokana na jinsia yao, kwamba ni wanawake, lakini pia kutokana na ulemavu wao, kwa hivyo hii yote inasababisha mtazamo hasi kwamba wanawake wenye ulemavu ni watu wasioweza, ni watu wa kusaidiwasaidiwa, wasioweza kujishughulisha. Lakini ya mwisho ni kutokana na umaskini walionao. Kwa hivyo vitu vyote hivi tunaviona ni changamoto ambazo wanawake wenye ulemavu wanazipata wanashindwa kufikia ndoto zao. Kwa hiyo sisi ni kuhakikisha wanawake hawa tunawajumuisha katika masuala mbalimbali, masuala ya kiuchumi, masuala ya kupambana ili kuhakikisha haki zote zinapatikana.”