Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mtu akitembea kwenye shamba la sola nchini Ufaransa

Safari ya kutokomeza uchafuzi wa hewa na kwanini dunia inaitegemea

Maxime Pontoire
Mtu akitembea kwenye shamba la sola nchini Ufaransa

Safari ya kutokomeza uchafuzi wa hewa na kwanini dunia inaitegemea

Tabianchi na mazingira

Nchi kadhaa hivi karibuni zimetangaza ahadi za kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wao wa hewa ukaa, na kuitokomeza kabisa hewa hiyo katika miaka ijayo. Tamko hilo limekuwa kilio cha kimataifa, kinachotajwa mara kwa mara kama hatua muhimu ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na uharibifu yanaousababisha.

Kutozalisha hewa ukaa ni nini na kwa nini ni muhimu?

Kimsingi, kutozalisha hewa ukaa kunamaanisha kuwa hatuongezi uzalishaji mpya wa hewa chafuzi kwenye anga. Uzalishaji mwingine unaweza kuendelea, lakini uende sanjari na kuondoa kiwango sawia hewani.

Hewa mbadala kama hii inayotokana na upepo ni muhimu katika kutokomeza uchafuzi wa hewa kwenye shamba Montenegro.
Unsplash/Appolinary Kalashnikova
Hewa mbadala kama hii inayotokana na upepo ni muhimu katika kutokomeza uchafuzi wa hewa kwenye shamba Montenegro.

 

Karibia nchi zote zimejiunga na Mkataba wa Paris wa kupambana na mabadiliko ya hali ya tabianchi, ambao unatoa wito wa kuweka viwango vya joto la ulimwengu kusalia nyuzi joto 1.5 ° C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda. Iwapo tutaendelea kuongeza uzalishaji unaosababisha mabadiliko ya tabianchi basi joto litaendelea kuongezeka zaidi ya nyuzi 1.5, na kufikia viwango vya kutishia maisha na vyanzo vya maisha ya watu kila mahali.

Hii ndio sababu idadi kubwa ya nchi zinaahidi kupunguza au kutozalisha kabisa hewa ukaa katika miongo michache ijayo. Ni kazi kubwa, inayohitaji hatua kabambe kuanzia sasa .

Lengo ni kutozalisha hewa ukaa ifikapo mwaka 2050. Lakini nchi pia zinahitaji kuonyesha jinsi gani zitakavyofikia lengo hilo. Jitihada za kufikia lengo hilo  lazima ziambatane na hatua za kukabiliana na hali halisi na mikakati ya kujenga mnepo , na uhamasishaji wa ufadhili kwa ajili ya nchi zinazoendelea.

Je ni vipi dunia inaweza kutokomeza uchafuzi wa hewa?

Habari njema ni kwamba kuna teknolojia ya kufikia lengo hilo na gharama yake si kubwa.

Jambo muhimu ni kukuza uchumi kwa kutumia nishati safi, kuachana na nishati ya mkaa ya mawe, gesi na mafuta kisukuku na badala yake  kutumia vyanzo vya nishati jadidifu kama ya upepo au ya jua (sola). Hii itapunguza sana uzalishaji wa hewa ukaa. Na pia nishati mbadala sio safi tu, lakini pia mara nyingi ni ya bei rahisi kuliko mafuta kisukuku.
 

Gari linalotumia umeme nchini Ujerumani
Unsplash/Marc Heckner
Gari linalotumia umeme nchini Ujerumani

 

Kuingia katika usafiri unaotumia nishati ya umeme jadidifu pia kutakuwa na jukumu kubwa katika kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi, isitoshe itasaidia kupunguza uchafuzi wa hewa katika miji mikubwa duniani. Magari ya umeme yanaendelea kushuka bei na yamekuwa yenye ufanisi zaidi, na nchi nyingi, ikiwemo zile zilizoahidi kutozalisha hewa ukaa zimependekeza mipango ya kumaliza uuzaji wa magari yanayotumia mafuta ya kisukuku.

Uchafuzi mwingine mbaya wa hewa  unatoka katika sekta ya kilimo (mifugo huzalisha kiwango kikubwa cha gesi ya methane, ambayo ni gesi chafuzi). Hizi zinaweza kudhibitiwa zaidi kwa kupunguza ulaji wa nyama na badala yake kula vyakula vya mimea zaidi. Hapa pia, ishara zinatia matumaini, kama kuongezeka kwa umaarufu wa "nyama za mimea" ambazo sasa zinauzwa katika migahawa mikuwa ya kimataifa ya chakula

Nini kitatokea katika uchafuzi uliosalia?

Kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi ni muhimu sana. Ili kufikia lengo la kutozalisha kabisa hewa chafuzi tunahitaji pia kutafuta mbinu za kuondoa hewa ukaa iliyoko angani.

Hapa tena, suluhu tunazo. Cha muhimu zaidi ni kwamba suluhu hizo zimekuwepo katika mazingira yetu kwa maelfu ya miaka. "Suluhisho hizi za asili" ni pamoja na misitu, ndizi, mikoko, udongo na misitu ya mwani, ambayo yote ina uwezo katika kunyonya hewa ukaa. Hii ndio sababu juhudi kubwa zinafanywa kote ulimwenguni kuokoa misitu, kupanda miti, na kukarabati maeneo ya mboji na mikoko, na pia kuboresha mbinu za kilimo.

Kurejesha mazingira ya asili kwa mfano hapa nchini Cuba kutasaidia kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi
UNDP
Kurejesha mazingira ya asili kwa mfano hapa nchini Cuba kutasaidia kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi

Nani anawajibika kufikia lengo la kutozalisha hewa chafuzi?

Sisi sote tunawajibika kama watu binafsi, kwa minajili ya kubadilisha tabia zetu na kuishi kwa njia ambayo ni endelevu zaidi, na ambayo ina madhara kidogo kwa sayari dunia, na kubadili muundo wa maisha ambao umependekezwa katika kampeni ya Umoja wa Mataifa ya chukua hatua sasa.

Sekta binafsi pia zinahitaji kuunga mkono juhudi hizi na kwa sasa zinafanya hivyo kupitia Mkataba wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa ambao husaidia wafanyabiashara kuzingatia malengo ya Umoja wa Mataifa ya mazingira na jamii.


Hilo ni wazi, hata hivyo, nguvu kuu ya kuendesha mabadiliko haya itafanywa katika ngazi ya serikali za kitaifa, kama vile kupitia sheria na kanuni za kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi. Serikali nyingi sasa ziko katika njia sahihi. Kufikia mapema 2021, nchi zinazowasilisha zaidi ya asilimia 65 ya uzalishaji wa hewa chafuzi na zaidi ya asilimia 70 ya uchumi wa ulimwengu zitakuwa zimetoa ahadi kubwa ya kupunguza hewa chafuzi ya ukaa.

Muungano wa Ulaya, Japani na Jamhuri ya Korea, pamoja na zaidi ya nchi nyingine 110, wameahidi kutozalisha hewa chafuzi ya ukaa  ifikapo mwaka 2050; na China inasema itafanya hivyo kabla ya mwaka 2060.

Je! Ahadi hizi ni zaidi ya hotuba za kisiasa tu?

Ahadi hizi ni ishara muhimu zenye nia nzuri ya kufikia lengo, lakini lazima ziungwe mkono na hatua za haraka na kabambe. Hatua moja muhimu ni kuweka mipango ya kina ya mchango wa hatua za kitaifa  NDCs. Mipango hii hufafanua malengo na hatua za kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi ndani ya miaka 5 hadi 10 ijayo. Ni muhimu katika muongozo wa uwekezaji sahihi na kuvutia ufadhili wa kutosha wa kifedha

Kufikia sasa, wanachama 186 wa Mkataba wa Paris wametengeneza mikakati ya kitaifa au NDCs. Mwaka huu, wanatarajiwa kuwasilisha mipango mipya au iliyosasishwa inayoonyesha nia kubwa na hatua za kuchukua.

Je kutozalisha hewa chafuzi kunawezekana?

Ndio! Hasa ikiwa kila nchi, jiji, taasisi ya kifedha na kampuni itanachukua mipango halisi ya kulekea kutozalisha hewa ukaa ifikapo mwaka 2050.

Kujikwamua kutoka kwenye janga la COVID-19 kunaweza kuwa hatua muhimu na nzuri ya mabadiliko. Wakati vichocheo vya uchumi vinaanza kufanyakazi, kutakuwa na fursa ya kweli ya kukuza uwekezaji wa nishati mbadala, majengo yenye kujali mazingira, uchukuzi unaozingatia hewa safi na hatua zingine ambazo zitasaidia kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi.

Serikali za kitaifa zina jukumu kubwa la kuleta mabadiliko ya kupunguza uchafuzi.
Unsplash/Daniel Moqvist
Serikali za kitaifa zina jukumu kubwa la kuleta mabadiliko ya kupunguza uchafuzi.

Lakini sio nchi zote ziko katika nafasi sawa kuathiri mabadiliko, sivyo?

Hiyo ni kweli kabisa. Wachafuzi wakuu, kama nchi za uchumi mkubwa duniani za G20, ambazo zinachangia asilimia 80 ya hewa chafuzi, zinahitaji kuongeza kiwango chao cha nia na kuchukua hatua.

Pia, kuzingatia kwamba juhudi kubwa zaidi zinahitajika kujenga mnepo katika nchi zilizo katika mazingira magumu na kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi; ambao wanachangia kidogo katika kusababisha mabadiliko ya tabianchi lakini wao hubeba mzigo mkubwa zaidi. Hatahivyo mikakati ya kujenga mnepo na hatua za kukabiliana na hali hiyo haipati fedha inayozihitaji.

Hata wakati zinalenga kufikia lengo la kutozalisha hewa ukaa , nchi zilizoendelea lazima zitimize ahadi yao ya kutoa dola bilioni 100 kila mwaka kwa ajili ya kupunguza, kukabiliana na kujenga mnepo katika nchi zinazoendelea.