Ukipokea wageni nyumbani kwako vaa barakoa kama mzungumzo wa hewa hautoshelezi- WHO

2 Disemba 2020

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO) limetoa mwongozo wa nne kuhusu uvaaji wa barakoa kama njia mojawapo ya kujikinga na virusi vya Corona vinavyosababisha COVID-19.
 

Vipengele vipya katika mwongozo huu mpya vinajumuisha aya ya ushauri kwa wapitisha maamuzi juu ya matumizi ya wahudumu wa afya wakiwemo wataalamu wa afya na udhibiti wa maambukizi, wasimamizi wa afya, wafanyakazi wa afya na wale wa kijamii wanaotoa huduma za afya.

WHO inasema marekebisho haya yanazingatia ushahidi wa kisayanasi na wa kivitendo wakati pia utafiti zaidi unafanyika.
Mathalani katika eneo la kijamii ambako kuna maambukizi, WHO inapendekeza matumizi ya barakoa za kitabibu katika hospitali, vituo vya afya na zahanati ilihali wananchi wavae barakoa za kawaida.

Katika maeneo ambako kunashukiwa kuwepo kwa maambukizi ya Corona kwenye jamii, wananchi wavae barakoa ndani, na wavae pia wanapokuwa nje iwapo hawawezi kuzingatia umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu.

Halikadhalika, watu wanapokuwa ndani ya jengo wavae barakoa, na “wanaweza wasivae iwapo tu hali ya mzunguko wa hewa ndani imefanyiwa tathmini na kuthibitishwa kuwa inatosheleza.”

Halikadhalika watu wanapokuwa nyumbani na wanapokea wageni, kama mzunguko wa hewa si wa kutosheleza basi wote wavae barakoa.

Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa pia linapendekeza pia watu wanapokuwa wanafanya mazoezi wasivae barakoa na pia watu wasivae barakoa zenye valvu.

Mara ya mwisho mwongozo wa WHO wa jinsi ya matumizi ya barakoa ulitolewa na kuchapishwa tarehe 21 mwezi Agosti mwaka huu wa 2020.

Tangu kuibuka kwa COVID-19 mwezi Machi mwaka huu, watu 63,360,234 wameambukizwa ugonjwa huo na kati yao hao 1,475,825 wamefariki dunia.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter