Mishahara ya watu yazidi kushuka duniani kisa? COVID-19:ILO 

2 Disemba 2020

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la kazi duniani ILO imesema janga la corona au COVID-19 limezidisha madhila kwa wafanyakazi ambao mishahara yao ilikuwa tayari chini ya kiwango cha chini kinachohitajika

Kwa mujibu wa ripoti hiyo katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa 2020 mishahara ya kila mwezi kwa mamilioni ya wafanyakazi duniani imeshuka zaidi au kutopanda kutokana na athari za COVID-19 katika theluthi mbili ya nchi zilizowasilisha takwimu zao kote duniani na hilo litaendelea kuleta shinikizo kubwa katika mishara kwa siku za usoni. 

Ripoti imeongeza kuwa waathirika wakubwa ni wanawake na wafanyakazi wa kipato cha chini. Zaidi ya hapo ripoti imesema na katika theluthi moja ya nchi zilizosalia ambako takwimu zinaonyesha ongezeko la mishahara ni kwa sababu idadi kubwa ya wafanyakazi wa kipato kidogo wamepoteza ajira na hivyo kutojumuishwa kwenye takwimu za mishahara. 

Ripoti hiyo ya mishahara kimataifa 2020/2021 inaonyesha pia athari haziko sawa kwani katika nchi 28 za Ulaya utafiti umebaini kwamba wanawake wamepoteza asilimia 8.1 ya kipato chao katika robo ya pili ya mwaka 2020 ikilinganishwa na asilimia 5.1 kwa wanaume. 

Pia watu wa kipato cha chini wamepoteza zaidi ujira wao ikilinganishwa na wafanyakazi wenye utaalam maalum, wenye kipato kikubwa au wanaoshikilia nyadhifa za uongozi. 

Mkurugenzi mkuu wa ILO Guy Ryder akizungumzia hali hii amesema “ Ongezeko la pengo la usawa lililosababishwa na COVID-19 linatishia jitihada za kutokomeza umasikini na kuleta utulivu katika masuala ya kijamii na kiuchumi na hii itakuwa na athari mbaya sana. Juhudi zetu  na mikakati ya kujikwamua lazima itoe kipaumbele kwa watu. Tunahitali sera bora za ajira ambazo zinazingatia uendelevu wa ajira na kuziba pengo la usawa. Na endapo tunataka kujijenga vyema basi pia ni muhimu kushughulikia masuala kama kwa nini ajira zenye thamani muhimu ya kijamii wakiwemo waalimu mara nyingi wanalipwa ujira mdogo.” 

Kiwango cha chini cha mishahara ILO inasema kimewekwa kwa asilimia 90 ya nchi wanachama wake lakini hata kabla ya COVID-19 duniani kote watu milioni 256 walikuwa wakilipwa chini ya kiwango cha chini cha mishara kilichowekwa. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter