Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naamka kila siku kwa matumaini ya kuleta mabadiliko japo kwa mtu mmoja:Mkimbizi Mahasin Khattab 

Wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wakiwasili kambi ya Atma, Idlib, Kaskazini magharibi mwa Syria.
WFP/Fadi Halabi
Wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wakiwasili kambi ya Atma, Idlib, Kaskazini magharibi mwa Syria.

Naamka kila siku kwa matumaini ya kuleta mabadiliko japo kwa mtu mmoja:Mkimbizi Mahasin Khattab 

Wahamiaji na Wakimbizi

 Kutana na mkimbizi kutoka Syria ambaye sasa anaishi kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Atma iliyoko karibu na mpaka wa Uturuki. Pamoja na madhila yote aliyopitia anapata faraja anapoweza kubadili maisha japo ya mkimbizi mmoja kwa ushauri nasaha anaotoa kwa maelfu ya wakimbizi kambini hapo

Kaskazini mwa Syria katika jimbo la Idlib kambi kubwa ya wakimbizi wa ndani ya Atma inayopatiwa msaada na mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, imefurika maelfu ya wanawake wanaume na watoto waliokimbia vita na miongoni mwao ni Mahasin Khattab mtaalam wa masuala ya saikolojia . 

Mahsin mwenye umri wa miaka 31 kazi yake kubwa ni kutoa ushauri nasaha kwa wakimbizi wa ndani kambini hapo na anaishi na watoto wake na mumewe mwenye ulemavu.“Kila siku naamka nikiwa na matumaini ya kuleta mabadiliko, mabadiliko katika maisha ya mtu mwenye uhitaji. Familia yangu na watoto wangu ni kila kitu kwangu, lakini kazi yangu inanitosheleza na kunipa furaha” 

Kila uchao Mahsini anatoka nakwenda kuzitembela familia za wakimbizi kambini hapo na kuzungumza nazo kuhusu shinikizo na msongo wanaoupata na kisha anawasaidia kwa ushauri nasaha, kuanzia wazazi na hata watoto waliopoteza wazazi wao vitani. “Ninapokutana na watu nasikiliza hadithi zao na kuhisi machungu yao, najaribu kuwapunguzia shinikizo na msongo wanaohisi.” 

Kwa kufanya hivyo Mahsini anasema anatoa faraja japo kidogo na kuwapunguzia machungu wakimbizi hao ambao maisha yao yamesambaratishwa na vita ,“Vita hivi vimekuwa na athari mbaya sana kwa watu, wote tunahitaji msaada wa kisaikolojia, licha ya rasilimali zetu ndogo , ni wajibu wetu kutoa msaada. Tunaishi ili kuleta tabasamu, kufuta machozi, kupunguza machungu na kuchagiza matumaini.” 

Umoja wa Mataifa unasema vita vya Syria ambavyo vimedumu miaka 10 sasa vimewaacha mamilioni ya watu wakihitaji msaada muhimu wa kisaikolojia mbali ya misaada mingine ya kibinadamu.