Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yazidisha makadirio ya mahitaji ya kibinadamu 2021 

Mwanamke aliyefurushwa akiwa ndani ya hema kwenye kambi ya muda, Gao inayohifadhi familia 300 waliokimbia makwao Tessit, Mali kufuatia mzozo.
© UNOCHA/Michele Cattani
Mwanamke aliyefurushwa akiwa ndani ya hema kwenye kambi ya muda, Gao inayohifadhi familia 300 waliokimbia makwao Tessit, Mali kufuatia mzozo.

COVID-19 yazidisha makadirio ya mahitaji ya kibinadamu 2021 

Masuala ya UM

Watu milioni 235 duniani kote watahitaji misaada ya kibinadamu na ulinzi mwakani 2021, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kufikiwa, amesema mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa misaada ya kibinadamu (OCHA) Mark Lowcock hii leo, akitaja fedha zinazohitajika kukidhi operesheni hizo kuwa ni dola bilioni 35. 

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video mjini Geneva, Uswisi Bwana Lowcock, amesema idadi hiyo ni rekodi kwa kuwa janga la ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19 limeongeza mahitaji zaidi na kuathiri watu ambao tayari walikuwa wamekimbia mizozo, majanga ya asili kama vile mabadiliko ya tabianchi huku baa la njaa nalo likinyelemea. 

“Hali ni ya kukatisha tamaa kwa mamilioni ya watu na imeacha Umoja wa Mataifa na wadau wake wakiwa wamezidiwa uwezo,” amesema mkuu huyo wa OCHA

Taswira imegubikwa na kiza kinene 

Amefafanua kuwa taswira inayoonekana sasa imegubikwa na kiza kinene kuwahi kushuhudiwa katika kukidhi mahitaji ya kibinadamu, “na hiyo ndio inaashiria jinsi gani COVID-19 imevuruga hali katika nchi ambazo tayari zilikuwa na hali tete duniani.” 

Bwana Lowcock ameongeza kuwa “tulidhani kuwa takribani watu milioni 170 dunani watahitaji msaada mwaka huu. Kuelekea 2021 tunadhani idadi itakuwa milioni 235, ongezeko hilo linachochewa bila shaka na COVID-19.” 

Wasichana wakiwa katika kambi ya Al Dhale'e ya wakimbizi wa ndani nchini Yemen.
YPN for UNOCHA
Wasichana wakiwa katika kambi ya Al Dhale'e ya wakimbizi wa ndani nchini Yemen.

Mshikamano ndio jawabu- Guterres 

Akipigia chepuo wito wa Bwana Lowcock wa mshikamano duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesihi dunia iwe na mshikamano na watu walio katika nyakati za uhitaji zaidi wakati huu ambapo janga la Corona linazidi kushika kasi. 

“Ijapokuwa mfumo wa kusambaza misaada ya kibinadamu imesambaza chakula, malazi, huduma za elimu na vifaa vingine muhimu kwa makumi ya mamilioni ya watu, janga bado halijafikia ukomo,” amesema Katibu Mkuu katika taarifa yake. 

Mwaka huu, tathmini ya kibinadamu duniani (GHO) imeweka mipango ya kufikia watu milioni 160 walio hatarini zaidi katika nchi 56, na iwapo mipango hiyo itafadhiliwa ipasavyo, itahitaji dola bilioni 35,” amesema Bwana Lowcock 

Nchi tajiri zinajipanga huku maskini zikiwa hazina mwelekeo 

Ametanabaisha kuwa wakati nchi tajiri zimewekeza dola trilioni 10 ili kupunguza athari za kiuchumi zitokanazo na COVID-19, na sasa wanaona kuna unafuu, hali si hiyo kwa nchi maskini zaidi duniani. 

“Janga la COVID-19 limetubukiza mamilioni ya watu kwenye umaskini na kuongeza zaidi mahitaji ya kibinadamu. Fedha za misaada zinahitajika ili kuondoa njaa, kutokomeza umaskini, kuhakikisha watoto wanaendelea kwenda shule na pia wanapatiwa chanjo,” amesema mkuu huyo wa OCHA. 

Halikadhalika amesema kuwa fedha taslimu zitatolewa kutoka fuko la dharura la Umoja wa Mataifa (CERF) ili kukabili ongezeko la vitendo vya ukatili dhid iya wanawake na wasichana vinayohusiana na uwepo wa COVID-19. 

Mwanamke akipokea matibabu kwenye kituo cha muda Hamdayet Sudan.
© UNFPA Sudan/Sufian Abdul-Mout
Mwanamke akipokea matibabu kwenye kituo cha muda Hamdayet Sudan.

Mabadiliko ya tabianchi, mizozo mipya ni mwiba zaidi 

Amegusia pia jinsi mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la viwango vya joto duniani vinazidi kuweka kiza katika mtazamo wa mahitaji ya kibinadamu mwaka 2021 “madhara yake yakiwa makubwa zaidi kwa nchi ambazo tayari zina changamoto kubwa za kibinadamu. Nchi 8 kati ya 10 zilizo hatarini kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi ni zile ambako mahitaji ya kibinadamu nayo ni makubwa.” 

Mizozo mipya nayo sambamba na ile ya zamani nayo imechangia pia katika ongezeko la mahitaji“mfano kuibuka kwa mizozo mipya kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa na amani. Tumeshuhudia bila shaka mzozo wa Nagorno-Karabakh, tumeshuhudia kaskazini mwa Msumbiji, tumeshuhudia Sahara Magharibi na hivi karibuni zaidi hali ya kutisha huko kaskazini mwa Ethiopia.” 

Mkuu huyo wa OCHA amesema cha kusikitisha mizozo hii mipya haijachukua nafasi ya mizozo ambayo imetatuliwa na kuwa na utulivu katika maeneo mengine.“Ni dhahiri mambo ni mabaya sasa kibinadamu yakichochewa na mizozo kama ilivyokuwa tulivyozungumza mwaka mmoja uliopita. 

Ziba ufa badala ya kusubiri kujenga ukuta 

Sambamba na kuzipatia jamii mbinu za kujinusuru na janga, Bwana Lowcock amesema Umoja wa Mataifa unasisitiza hatua za kujikinga badala ya kusubiri kuchukua hatua. 

Ametaja hatua hizo zilijumuisha kulipatia fedha shirika la afya la Umoja wa Mataifa (WHO) mwezi Februari mwaka huu pindi tu janga la Corona lilipobainika ili kuhakikisha kuwa nchi maskini zaidi zinapata vifaa vya kujikinga na COVID-19. 

Halikadhalika, makumi ya maelfu ya manusura wa mafuriko Bangladesh walipokea msaada na fedha ili kusaidia mahitaji yao wakati wa mafuriko na kujipatia njia za kipato. 

Amesema kuwa hatua hizo za kinga zilipunguza mahitaji makubwa ambayo yangalihitajika iwapo wangalisubiri kwanza madhara makubwa yatokee ndio waanze kutoa msaada. 

Mkuu huyo wa OCHA amefananisha hatua hizo kuwa ni sawa na kutoa kikonyo cha mmea kwenye shina kabla hakijakomaa na kumaliza nguvu mmea mzima na ndio hatua mujarabu.