Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Theluthi mbili ya watoto wenye umri wa kwenda shule duniani hawana huduma ya intaneti nyumbani-Ripoti  

Wanafunzi wengi katika maeneo mengo mji wa Ahavaz, Iran hawawezi kushiriki masomo mtandaoni.
UNICEF
Wanafunzi wengi katika maeneo mengo mji wa Ahavaz, Iran hawawezi kushiriki masomo mtandaoni.

Theluthi mbili ya watoto wenye umri wa kwenda shule duniani hawana huduma ya intaneti nyumbani-Ripoti  

Utamaduni na Elimu

Muungano wa kimataifa wa mawasiliano ITU na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF zinataka uwekezaji wa haraka ili kuziba pengo la kidijitali ambalo kwa sasa linawazuia watoto na vijana kupata ujifunzaji bora wa kidijitali na fursa mtandaoni. 

Theluthi mbili ya watoto wenye umri wa kwenda shule duniani au watoto bilioni 1.3 wenye umri wa miaka 3 hadi 17 hawana intaneti nyumbani mwao, inaeleza ripoti mpya ya UNICEF na ITU iliyotolewa hii leo mjini New York na Marekani. 

Ripoti hiyo kwa jina, Ni watoto na vijana wangapi wana mtandao wa intaneti nyumbani? inabainisha pia ukosefu wa upatikanaji wa intaneti kati ya vijana wenye umri wa miaka 15-24, saw ana watoto milioni 759 au asilimia 63 wakiwa hawajaunganishwa na intaneti nyumbani. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietha Fore anasema, "Kwamba watoto na vijana wengi hawana mtandao wa inteneti nyumbani ni zaidi ya pengo la kidijitali, ni korongo la kidijitali. Ukosefu wa inatenti hauzuii tu uwezo wa watoto na vijana kuungana mtandaoni. Inawazuia kushindana katika uchumi wa kisasa. Inawatenga na ulimwengu. Na katika tukio la kufungwa kwa shule, hali ambayo sasa inakabiliwa na mamilioni kwa sababu ya coronavirus">COVID-19, inawasababishia kukosa elimu. Kuweka wazi: Ukosefu wa ufikiaji wa mtandao wa intaneti unagharimu hatima ya kizazi kijacho. " 

Karibu robo ya wanafunzi bilioni moja ulimwenguni kote bado wameathiriwa na kufungwa kwa shule kutokana na COVID-19, na kulazimisha mamilioni ya wanafunzi kutegemea ujifunzaji nje ya shule hususani kupitia mitandao.  Kwa wale ambao hawana ufikiaji wa mtandao, elimu haiwezi kufikiwa. Hata kabla ya janga hilo, kundi la vijana ambalo linaongezeka, linahitaji kujifunza ujuzi unaohamishika, wa kidijitali, wa kazi maalum na ujasiriamali ili kushindana katika uchumi wa karne ya 21.  

"Kuunganisha wakazi wa vijijini katika intaneti bado ni changamoto kubwa." Anasema Katibu Mkuu wa ITU, Houlin Zhao. 

Ijapokuwa takwimu za namba katika ripoti ya UNICEF-ITU zinaonesha picha ya kutisha, hali hiyo inaweza kuwa mbaya zaidi kwa sababu kadhaa, kama vile kumudu bei, usalama na viwango vya chini vya ujuzi wa kidijitali. Kulingana na data ya hivi karibuni ya ITU, ujuzi mdogo wa kidijitali unabaki kizuizi kwa ushiriki wa maana katika jamii ya kidijitali, wakati simu ya rununu na upatikanaji wa mtandao unabaki kuwa ghali sana kwa wengi katika ulimwengu unaoendelea kwasababu ya matokeo ya tofauti kubwa katika nguvu ya ununuzi. 

Hofu ya UNICEF na ITU ni kuwa, hata pale ambapo watoto wana intaneti nyumbani, wanaweza wasiweze kuitumia kwa sababu ya shinikizo la kufanya kazi za nyumbani au kufanya kazi, ukosefu wa vifaa vya kutosha katika kaya, wasichana wanaruhusiwa kupata intaneti kidogo au wasiruhusiwe kabisa, au ukosefu wa uelewa ya jinsi ya kupata fursa mtandaonii. Pia kuna masuala yanayohusiana na usalama mtandaoni kwani wazazi wanaweza kuwa hawajajitayarisha vya kutosha kuweka watoto wao salama.