Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huwezi kuyavalia barakoa mabadiliko ya tabianchi, pia hayana chanjo-Andrew Harper 

Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya changamoto zinazoikabili dunia. Mathalani ukanda wa Sahel kusini mwa jangwa la Sahara.
© UNDP Mauritania/Freya Morales
Mabadiliko ya tabianchi ni moja ya changamoto zinazoikabili dunia. Mathalani ukanda wa Sahel kusini mwa jangwa la Sahara.

Huwezi kuyavalia barakoa mabadiliko ya tabianchi, pia hayana chanjo-Andrew Harper 

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, kesho Jumatano likifanya mkutano wa ngazi ya juu kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wakimbizi na wakimbizi wa ndani, pamoja na wengine walio katika mazingira hatarishi kote, mshauri maalumu wa UNHCR kuhusu mabadiliko ya tabianchi Andrew Harper amesema dunia inapaswa kuchukua hatua kali zaidi kwani mabadiliko ya tabia nchi huwezi kuyavalia barakoa. 

Kuelekea tukio hili la kesho linalolenga kutafuta namna bora za kushughulikia athari za mabadiliko ya tabiachi kwa wakimbizi, mshauri maalumu wa UNHCR kuhusu mabadiliko ya tabianchi Andrew Harper amesema mabadiliko ya tabianchi, vichocheo vya migogoro na COVID-19 vimeufundisha ulimwengu kuhusu kushughulikia dharura za ulimwengu.  

Bwana Harper anasema, “asilimia 84 ya wakimbizi duniani wako katika nchi zinazoendelea. Na hizi ndizo nchi ambazo zina uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi, iwe ni jangwa, matukio mabaya ya kimbunga au kuongezeka kwa dhoruba." 

Akirejelea janga la COVID-19, Harper amesema, "kwa bahati mbaya, mabadiliko ya tabianchi huwezi kuyavalia barakoa na hakuna chanjo dhidi yake. Kwa hivyo, tunahitaji kuchukua hatua kali zaidi kukabiliana nayo.” 

Pia Bwana Harper amesema, "tuna uwajibikaji, jukumu, kufanya zaidi kuongeza utayari, ulinzi, msaada wa kukabiliana, sio tu kwa wale watu ambao tayari wamekimbia makazi yao, lakini wale watu ambao watazidi kuathirika siku za usoni. " 

Tukio hilo la ngazi ya juu kuhusu madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa wakimbizi, pamoja na mambo mengine, linalenga kusukuma hatua imara za ulimwengu katika kupambana na suala hili.