Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu kufurushwa kunaendelea Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji kutokana na ukosefu wa usalama.  

Kundi la watu waliokimbia machafuko katika wilaya za Cabo Delgado wamewasili katika mji mkuu wa jimbo la Pemba
IOM/Matteo Theubet
Kundi la watu waliokimbia machafuko katika wilaya za Cabo Delgado wamewasili katika mji mkuu wa jimbo la Pemba

Watu kufurushwa kunaendelea Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji kutokana na ukosefu wa usalama.  

Amani na Usalama

IOM mjini Maputo Msumbiji hii leo imeeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya kuendelea kufurushwa kwa watu katika eneo la kaskazini mwa Msumbiji kutokana na ukosefu wa usalama katika jimbo la Cabo Delgado.  

IOM inaripoti kuwa katika mwezi uliopita kuanzia tarehe 28 Oktoba hadi 25 Novemba,  zaidi ya watu 45,000 walitoroka wilaya ya kaskazini ya Muidumbe kwa sababu ya mashambulio mengi katika maeneo kadhaa. Watu wengine walikuwa wamehama makazi yao, wakati wengine walikuwa tayari wamehama makazi yao na tena wakilazimika kukimbia. 

"Kufurushwa kunaongezeka kaskazini mwa Cabo Delgado wakati mashambulio kwa raia yanaendelea, tuna wasiwasi sana juu ya hali hii na tunatoa msaada wa kibinadamu kwa kadri tuwezavyo. Familia zilizohamishwa ziko hatarini sana na msaada zaidi unahitajika ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu." Ameeleza Mkuu wa Ujumbe wa IOM Msumbiji Laura Tomm-Bonde. 

Zaidi ya watu 37,000 ya wale waliokimbia makazi yao kutoka Muidumbe, takriban kilomita 100 kutoka mpaka wa Msumbiji na Tanzania, walisafiri kaskazini kwenda wilaya ya Mueda. Wengine 5,000 walihamia kusini hadi Montepuez na watu 3,000 kuelekea mji mkuu wa mkoa Pemba kwa njia ya barabara. 

Ufuatiliaji wa waliotawanywa uliofanywa na IOM unaripoti kuwa takribani watu 424, 000 walihama makazi yao kufikia mwishoni mwa mwezi Septemba, nyongeza ya asilimia 17 kutoka mwezi uliokuwa umetangulia. Kati ya wote waliohamishwa, zaidi ya 144,000 wako katika maeneo ambayo ni ngumu kufikiwa kutokana na wasiwasi wa usalama. 

Mmoja wa watu nane kutoka familia moja ambao walikimbia kupitia misituni kwa miguu mnamo mwezi Julai kabla ya kupata usafiri kuelekea katika mji mkuu wa jimbo, Nlabite Chafim anasema, "tulilazimika kuondoka katika eneo letu kutokana na mashambulio mengi, na kuhamia mji wa Pemba, mpwa wangu alishuhudia wazazi wake wakiuawa, na sasa hayuko kama alivyokuwa." 

IOM inatoa msaada wa haraka kwa watu waliofurushwa kuunga mkono hatua za kibinadamu za Serikali ya Msumbiji. Msaada huo ni pamoja na vifaa vya makazi, mgawanyo wa vitu vya nyumbani, na uanzishwaji wa maeneo ya makazi yao na uratibu wa utoaji wa huduma za kimsingi. Mbali na afya ya akili na msaada wa kisaikolojia, IOM pia inawezesha upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha na huduma za ulinzi.