Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madagascar wanateseka kwa njaa, WFP yaingilia kati kuokoa maisha. 

Athari za pamoja za ukame, COVID-19 na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumedhoofisha zaidi hali ya uhakika wa chakula na lishe ya watu wa kusini mwa Madagascar.
WFP/Tsiory Andriantsoarana
Athari za pamoja za ukame, COVID-19 na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama kumedhoofisha zaidi hali ya uhakika wa chakula na lishe ya watu wa kusini mwa Madagascar.

Madagascar wanateseka kwa njaa, WFP yaingilia kati kuokoa maisha. 

Tabianchi na mazingira

Njaa imeongezeka katika eneo la kusini la Madagascar, mfululizo wa miaka ya ukame inazidisha mateso ya maelfu ya watu, kuharibu mavuno na kuzuia watu kupata chakula, limeeleza shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP.  

WFP kupitia taarifa yake kwenda kwa vyombo vya habari iliyotolewa hii leo mjini Geneva Uswisi, imesema nusu ya wakazi wa eneo hilo la kusini mwa Madagascar, ambao ni watu milioni 1.5, wanakabiliwa na hali ya "shida" au "dharura" na wanahangaika kuweka chakula kwenye meza zao. 

"Idadi ya watu walio katika uhitaji ni mara tatu ya ile iliyotarajiwa katikati ya mwaka kwani hali imekuwa mbaya zaidi na watu hao wameenea katika wilaya 10. Watu hawa wenye njaa wengi wao wakiwa wanawake na watoto wanahitaji msaada wa haraka wa chakula na lishe. Hali hiyo inatia wasiwasi sana. Njaa na utapiamlo tunaona ni matokeo ya mavuno yaliyoharibiwa kwa miaka mitatu." Imeeleza WFP. 

Shirika hilo la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa lina mipango ya kuwasaidia takribani watu 891,000 ambao wengi wao wako hatarini hadi mwezi Juni mwaka 2021.  

Aidha WFP imesema kadri idadi ya wenye njaa inavyoongezeka, ndivyo idadi ya familia zinazopambana na kukabiliana na shida zinavyoongezeka ikiwa ni pamoja na kula vyakula visivyofaa na kuuza vitu vyao thamani kama vyombo vya jikoni na vifaa vya shamba. 

Karibia nusu ya watoto chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo wa muda mrefu. Tathmini mwezi uliopita katika wilaya ya kusini ya Amboasary, eneo lililoathiriwa zaidi ilionyesha njaa ililazimisha robo tatu ya watoto kuacha shule ili waweze kuwasaidia wazazi wao kutafuta chakula. 

Hatua za WFP 

WFP ilianza kutoa msaada wa chakula cha dharura kuokoa maisha tangu mwishoni mwa mwezi Septemba, na kufikia zaidi ya 100,000 wa Amboasary iliyoathiriwa zaidi ndani ya siku chache. Mgawanyo wa chakula ulikuwa hususani kwa watoto wenye utapiamlo na wazee.  

WFP pia inatoa msaada kwa takribani watu 576, 000 katika maeneo mengine yaliyoathiriwa na ukame katika wilaya za kusini mwa Madagascar hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu wa 2020.  

Hata hivyo wakati WFP ikipambana na athari za ukame huo, nayo inakabiliwa na ukame wa pesa kwa miezi sita ijayo kwa kiasi cha dola milioni 37.5 za kimarekani.