Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo kutoka UN yamwezesha Veneranda kupata baiskeli sasa kufikia wakulima wengi zaidi 

Veneranda Hamisi, mnufaika wa mafunzo yanayoendeshwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa mkoani Kigoma nchini Tanzania.
UN News
Veneranda Hamisi, mnufaika wa mafunzo yanayoendeshwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa mkoani Kigoma nchini Tanzania.

Mafunzo kutoka UN yamwezesha Veneranda kupata baiskeli sasa kufikia wakulima wengi zaidi 

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkoani Kigoma nchini Tanzania, mafunzo yanayotolewa na mashirika ya Umoja wa Matafa likiwemo lile la chakula na kilimo , FAO, mpango wa chakula duniani, WFP na maendeleo ya mitaji, UNCDF  kwa wakulima wawezeshaji yamefungua nuru ya mmoja wao na hadi kuwezeshwa na shirika hilo ili aweze kusaidia wakulima wenzake. 

Mkulima mwezeshaji huyo, Veneranda Hamisi kutoka halmashauri ya Kasulu Vijijini kata ya Rusesa, kijiji cha Kasangezi alipatiwa mafunzo kama vile mbinu za kilimo bora, kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi, elimu ya hifadhi ya mazao pamoja na elimu ya fedha na masoko. 

Baada ya kupata mafunzo ya awali kupitia programu ya pamoja ya Kigoma, KJP, mwaka 2018, veneranda kupitia Kikundi chake na majirani wanaomzunguka ameweza kuwafundisha wanakikundi wenzake yote yale aliyoyapata katika mafunzo ili kuleta tija ya mazao makuu yaliyopo katika KJP ambayo ni mahindi, maharage na mihogo. 

Binafsi nimeweza kupata mafanikio katika kuongeza uzalishaji toka gunia 1 la mahindi toka kwenye eka 1 na kufikia gunia 15 baada ya kutumia mbegu bora za mahindi, na kufuata kanuni bora za kilimo,” anajivunia Veneranda. 

Hata hivyo hayo si mafanikio pekee kwani sasa amepatiwa baiskeli Ili kurahisisha kuwafikia wakulima wengi zaidi mbali na wanakikundi wenzake walio karibu naye. 

Matarajio ya Bibi veneranda ni kuwagfikia wakulima wenzake katika kuwapatia huduma za ushauri katika kilimo kama alivyofundishwa kupitia mradi wa pamoja wa Kigoma unaofadhiliwa kwa pamoja na serikali ya Tanzania kwa msaada wa serikali ya Norway. 

Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma ilianza mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayohusika ni pamoja na lile chakula na kilimo, FAO, mpango wa chakula, WFP, kituo cha biashara cha kimataifa, ITC na lile la maendeleo ya mitaji, UNCDF.