Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila sekunde 100, mtoto 1 aliambukizwa VVU mwaka jana-UNICEF 

Mwanamke mwenye VVU anapokea dawa kwa ajili ya mtoto wake wa umri wa siku tatu katika hospitali huko Ouagadougou, Burkina Faso.
UNICEF/Frank Dejongh
Mwanamke mwenye VVU anapokea dawa kwa ajili ya mtoto wake wa umri wa siku tatu katika hospitali huko Ouagadougou, Burkina Faso.

Kila sekunde 100, mtoto 1 aliambukizwa VVU mwaka jana-UNICEF 

Afya

Takribani kila dakika moja na sekunde 40, mtoto au kijana chini ya umri wa miaka 20 alikuwa anaambukizwa Virusi Vya UKIMWI, VVU mwaka jana 2019, na kufanya idadi ya watoto wanaoishi na VVU kufikia milioni 2.8, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema katika ripoti yake iliyotolewa leo mjini New York Marekani na Johannesburg Afrika Kusini. 

Ripoti hiyo, kwa jina Ufikiriaji mpya ushughulikiaji VVU wenye mnepo kwa ajili ya watoto, barubaru na wajawazito wanaoishi na VVU, inaonya kuwa watoto wanaachwa nyuma katika vita dhidi ya VVU. 

Jitihada za kuzuia na matibabu kwa watoto yanabaki kuwa ya chini kabisa miongoni mwa watu muhimu walioathirika. Katika mwaka 2019, si zaidi ya nusu ya watoto watoto ulimwenguni kote walipata matibabu ya kuokoa maisha, ambayo yanazorota kwa akina mama asilimia 85, na watu wote wazima wanaoishi na VVU asilimia 62. Takribani watoto 110, 000 walifariki kwa UKIMWI katika mwaka huo wa 2019, imeeleza taarifa ya UNICEF.  

Ripoti imesema licha ya maendeleo kadhaa katika mapambano ya muda mrefu dhidi ya VVU na UKIMWI, tofauti kubwa za kikanda zinaendelea miongoni mwa watu wote, hasa kwa watoto.  

"Hata wakati ulimwengu unapambana katikati ya janga linaloendelea ulimwenguni, mamia ya maelfu ya watoto wanaendelea kupata mateso ya janga la VVU," Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema na kuongeza, “bado hakuna chanjo ya VVU. Watoto bado wanaambukizwa kwa viwango vya kutisha, na bado wanakufa kutokana na UKIMWI. Hii ilikuwa hata kabla ya COVID-19 kukatiza huduma muhimu za matibabu ya VVU na kinga kuweka maisha mengi zaidi katika hatari." 

COVID-19 nayo imeathiri 

Katika miezi ya Aprili na Mei, sanjari na kufungwa kwa mipaka, matibabu ya VVU kwa watoto na upimaji wa virusi kwa watoto katika nchi zingine ulipungua kati ya asilimia 50 hadi 70, na uanzishwaji mpya wa matibabu ulipungua kwa asilimia 25 hadi 50. 

Takwimu za ziada za 2019 zilizojumuishwa katika ripoti: 

Watoto 150,000 wenye umri wa miaka 0-9 walikuwa wameambukizwa VVU hivi karibuni, na kufanya idadi ya watoto katika umri huu wanaoishi na VVU kufikia milioni 1.1. 

Vijana 170,000 wenye umri wa miaka 10-19 waliambukizwa VVU hivi karibuni, na kufanya idadi ya vijana wanaoishi na VVU kufikia milioni 1.7. 

Wasichana barubaru 130,000 waliambukizwa VVU mnamo 2019, ikilinganishwa na wavulana barubaru 44,000. 

Jumla ya vifo vinavyohusiana na UKIMWI vya watoto na vijana vilikuwa 110,000; 79,000 wenye umri wa miaka 0-9 na 34,000 wenye umri wa miaka 10-19. 

Ufikiaji wa akina mama wa tiba ya kurefusha maisha kuzuia maambukizi ya virusi kwa watoto wao uliongezeka ulimwenguni hadi asilimia 85 na utambuzi wa mapema wa watoto ulifikia asilimia 60. 

Idadi ya wanawake wajawazito wanaoishi na VVU ilikuwa milioni 1.3; watoto wanaokadiriwa kuwa 82,000 walio chini ya umri wa miaka mitano waliambukizwa wakati wa ujauzito au wakati wa kuzaa na 68,000 waliambukizwa wakati wa kunyonyesha. 

Ripoti hiyo inazitaka serikali zote kulinda, kudumisha na kuharakisha maendeleo katika kupambana na VVU miongoni mwa watoto kwa kudumisha huduma muhimu za afya na kuimarisha mifumo ya afya.