Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaachia dola milioni 25 kwa ajili ya wanawake wanaopambana na unyanyasaji wa kijinsia  

Mwanamke akiwa amembeba binti yake katika kituo cha Wisdom kilichopo eneo la Gurei mjini Juba nchini Sudan kusini baada ya kupigwa na mumewe.
© UNICEF/Albert Gonzalez Farran
Mwanamke akiwa amembeba binti yake katika kituo cha Wisdom kilichopo eneo la Gurei mjini Juba nchini Sudan kusini baada ya kupigwa na mumewe.

UN yaachia dola milioni 25 kwa ajili ya wanawake wanaopambana na unyanyasaji wa kijinsia  

Haki za binadamu

Mkuu ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya dharura, OCHA, Mark Lowcock hii leo mjini New York Marekani ametangaza kuwa zimetolewa dola za kimarekani milioni 25 kutoka kwenye mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF, kusaidia mashirika yanayoongozwa na wanawake ambayo yanapambana dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Fedha hizo zimekwenda kwa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA na lile la wanawake UN Women ambao wameombwa kupeleka angalau asilimia 30 ya fedha kwa mashirika yanayoendeshwa na wanawake ambayo yanazuia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, na kusaidia wahanga na waathirika kupata huduma za matibabu, uzazi wa mpango, ushauri wa kisheria, usalama, huduma za afya ya akili na ushauri. 

Bwana Lowcock amesema, "janga la COVID-19 limesaidia kufunua kiwango kamili cha ukosefu wa usawa wa kijinsia wakati wa kuunda mazingira ambayo yanatishia kurudisha nyuma maendeleo ambayo yamepatikana. Kila mtu ambaye ana nia ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake lazima azungumze. Halafu wale walio na namna ya kufanya hivyo wanahitaji kuweka pesa zao mahali ambapo vinywa vyao viko. Mahitaji ya wanawake na wasichana katika mazingira ya kibinadamu yanaendelea kupuuzwa na kufadhiliwa kidogo. Ni uwekezaji mzuri na ni jambo sahihi kufanya. Tunaweza tu kufanikiwa kwa kupata njia ya kutoka kwenye janga hili ikiwa tutaleta kila mtu pamoja nasi.” 

UNFPA itapokea dola milioni 17 na pia dola milioni 8 zitaenda kwa UN Women. Mashirika hayo yataamua  ni wapi na jinsi pesa zitatumika na wameombwa kupitisha angalau asilimia 30 ya ufadhili kupitia mashirika yanayoongozwa na wanawake yanayoshughulikia unyanyasaji wa kijinsia. 

"Ni wakati wa kusema 'Inatosha' kwa unyanyasaji wa kijinsia na kutanguliza haki na mahitaji ya wanawake na wasichana katika mizozo ya kibinadamu.” Amesema Dkt Natalia Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa, UNFPA. 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema, "Viwango vya juu vya unyanyasaji wa kijinsia ambao wanawake na wasichana wanapata, haswa katika nchi ambazo zina shida na wanaohitaji msaada wa kibinadamu, bado ni moja ya dhuluma kubwa katika ulimwengu wetu."  

Tangazo hili la ufadhili limekuja mwanzoni mwa Siku 16 za kuhamasisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, kampeni ya kimataifa ya kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana ambayo inaanza kila mwaka kuanzia 25 Novemba, Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake, hadi tarehe 10 Desemba, Siku ya Haki za Binadamu.