Chonde chonde Brazil chunguzeni mauaji ya João Alberto Silveira Freitas

24 Novemba 2020

Mauaji ya João Alberto Silveira Freitas, raia wa Brazil mwenye asili ya Afrika kwenye mji wa Porto Alegre kusini mwa Brazil ni jambo la kutisha lakini pia cha kusikitisha ni dhihirisho la ukatili na ghasia zinazokumba watu wenye asili ya Afrika.
 

Hiyo ni kauli ya Ravina Shamdasani, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa aliyoitoa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kufuatia mauji hayo yaliyofanywa na walinzi wawili binafsi.

Bi. Shamdasani amesema tukio hilo la kuchukiza ambalo limetokea kwenye mkesha wa siku ya kuhamasisha kuhusu watu weusi nchini Brazil, linapaswa kulaaniwa na kila mtu.

“Mamlaka za serikali zinapaswa kuwajibika na kukikiri uwepo wa tatizo hilo la ubaguzi nchini Brazil, kwa kuwa hiyo ndio hatua ya kwanza ya kusaka suluhu ya tatizo hilo,” amesema afisa huyo wa OHCHR.

Mfumo wa kibaguzi, ubaguzi wa rangi na ghasia dhidi ya watu wenye asili ya Afrika nchini Brazil umerekodiwa kwenye takwimu rasmi hali inayodokeza kuwa idadi ya mauaji ya wabrazil wenye asili ya Afrika ni kubwa kuliko mauaji ya makundi mengine.

Takwimu pia zinaonesha kuwa wabrazil wenye asili ya Afrika, wakiwemo wanawake, idadi yao ni kubwa zaidi magerezani.

“Tunaelewa kuwa uchunguzi unafnayika juu ya kifo cha Silveira Freitas. Unapaswa kuwa wa haraka, kina, huru, usiogemea upande wowote na wa uwazi. Jambo hili linapaswa kuzingatia haki, ukweli na kupatia fidia familia yake,” amesema Bi, Shamdasani.

Ametoa wito pia kwa mamlaka kuchunguza madai yooyte ya matumizi yasiyo ya lazima ya nguvu dhidi ya watu waliokuwa wanaandamana kusaka washukuwa wa mauaji hayo wawajibishwe.

OHCHR imesema kuwa hali ya zamani ya ubaguzi nchini Brazil bado inaendelea kama ilivyo katika jamii zingine, “wabrazil weusi wanavumilia ubaguzi wa kimfumo, kutengwa, kuenguliwa na ukatili na katika matukio mengi athari zake ni hatari.”

Bi. Shamdasani amesema weusi hao wameenguliwa hata kwenye mifumo ya kupitisha uamuzi na taasisi nyinginezo.

Ili kukabiliana na hali hiyo, Bi. Shamdasani amesema ni lazima kufanyike haraka marekebisho ya sheria, ikiwemo kuwepo na upendeleo maalum kwa kundi hilo iwapo itahitajika kufanya hivyo ili nao wapate fursa.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud