Dola milioni 2 zahitajika haraka kuepusha janga la kibinadamu jimbo la Lac Chad:IOM 

24 Novemba 2020

Wiki hii shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limetoa ombi la dola milioni 2 ili kuhakikisha linaendelea kuwa na fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha kwa watu waliohatarini zaidi na jamii zinazowahifadhi. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo shirika hilo limesema miongoni mwa msaada huo ni ule wa mahitaji ya dharura na maandalizi na kuimarisha program za upunguzaji wa hatari za majanga. 

Mapema mweszi huu mamlaka katika jimbo la Lac nchini Chad walilitaarifu shirika la IOM kuhusu mafuriko makubwa katika maeneo ya yote ya Fouli na Kaya yaliyosababishwa na kufurika kwa ziwa Chad sababu ya mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha na maeneo hayo ndiyo yanayohifadhi maelfu ya wakimbizi wa ndani waliotawanywa na vita na mabadiliko ya tabianchi. 

IOM inasema jimbo la Lac linakabiliwa na athari za majanga makubwa mawili ambayo ni usalama na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ambayo yote yamewalazimisha watu zaidi ya nusu wa jimbo hilo kufungasha virago na wengi bila huduma zozote za msingi. 

Akizungumzia hali hiyo mkuu wa IOM nchini Chad Anne Schaefer amesema “Mafuriko ya ghafla ambayo yanaendelea yanaweza kuwafanya wanavijiji zaidi kuzikimbia nyumba zao na kusaka hifadhi katika vijiji vya jirani ambako tayari rasilimali na mahitaji ya lazima ni haba. Kiwango cha maji kinapoendelea kuongezeka katika baadhi ya maeneo ambako tuliweza kusaidia sasa yatakuwa hayafikiki na hivyo kuwaacha maelfu ya watu bila msaada wa lazima wa kuokoa maisha na hilo litakuwa janga kubwa.” 

Ameongeza kuwa na athari za majanga hayo mawili ni kutawanywa kwa watu zaidi ya 360,000 ambayo zaidi ya nusu ya watu wa jimbo hilo. 

Yacoub Mazhamat mkuu wa eneo la Fouli kawenye jilo hilo la Lac amesema “Watu wetu wanakabiliwa na migogo mingi, lakini ongezeko la kina cha maji ambalo tumelishuhudia katika siku za karibuni linatishia kaya zaidi ya 18,000 wakiwemo wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahifadhi.” 

Kwa mujibu wa IOM mafuriko hayoa pia yanaleta hatari ya magonjwa ya mlipuko yatokanayo na maji kama kipindupindu na malaria. 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter