Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yawa mzigo mkubwa kwa wakimbizi Misri 

Mradi wa UNDP na serikali ya Misri wa kutengeneza barakoa
UNDP Misri
Mradi wa UNDP na serikali ya Misri wa kutengeneza barakoa

COVID-19 yawa mzigo mkubwa kwa wakimbizi Misri 

Wahamiaji na Wakimbizi

Kabla ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19, idadi kubwa ya wakimbizi nchini Misri walikuwa tayari katika hali ya hatari katika kujikwamua maisha yao. Sasa na janga la Corona, wengi wao wamepoteza vyanzo vyao vya kipato na wanahaha kukimu mahitaji yao ya msingi. 

Miongoni mwao ni Zahra, ambaye akiwa kwenye chumba chake kimoja anamoishi na wanawake wengine watatu, macho yake yanatizama simu yake ya kiganjani. Matarajio yake ni kupokea simu kutoka kwa mwajiri yeyote mtarajiwa, jambo ambalo amekuwa akifanya hivyo kwa takribani miezi mitatu sasa. 

Zahra, mwenye umri wa miaka 20, ni raia wa Eritrea, na aliwasili bila mlezi yeyote miaka minne iliyopita. Akiwa mtoto alipokea msaada wa kifedha kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, sambamba na msaada wa elimu na kisaikolojia kutoka wadau wa shirika hilo. 

Hata hivyo, baada ya kuwa mtu mzima, analazimika kutumia stadi alizopata ili kujisaidia mwenyewe. “Nafanya kazi za kawaida tu angalau mkono uende kinywani. Nimewahi kuwa mhudumu kwenye mgahawa na hata kuwa mfanyakazi wa majumbani.” 

N’gombe wa maskini hazai 

Wahenga wanasema, n’gombe wa maskini hazai, na ndivyo ilivyokuwa kwa Zahra kwani harakati zake za kujipatia kipato ziliingia doa baada ya kuugua COVID-19, gonjwa ambalo linatarajiwa kupeleka mrama maisha ya wakimbizi wengi katika nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. 

Kwa Zahra, kama ilivyo kwa wakimbizi 258,862 waliosajiliwa kuwa wakimbizi na wasaka hifadhi nchini Misri, madhara ya COVID-19 kwenye maisha yao ni makubwa kupindukia na ni dhahiri. 

“Sikuweza kulipa pango kwa miezi mitatu mfululizo na nilikuwa naishi kwa hofu kubwa kila uchao. Hakuna mwenye nyumba yeyote ambaye anayeweza kuvumilia kutolipwa pango kwa muda mrefu,” amesema Zahra ambaye hali yake ya kutoweza kulipa pango si tofauti na wenzake watatu anaoishi nao. 

UNHCR na wadau wajitokeza kunusuru wakimbizi 

Mwezi Septemba, mwaka huu, Zahra alikuwa miongoni mwa wakimbizi na wasaka hifadhi 1,495 waliokuwa hatarini zaidi kutoka Syria, Sudan, South Sudan, Eritrea, Ethiopia na Somalia, ambao walipatiwa msaada wa muda mfupi kama sehemu ya mpango wa UNHCR ya kuongeza jitihada zake za kupunguza athari za kiuchumi na kijamii za COVID19 kwa makundi hayo. 

Walipatiwa fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kujisafi sambamba na kusaidia wazee na wagonjwa. 

“Sifahamu ningalifanya nini iwapo nisingalikuwa nimepata msaada huo,” amesema Zahra akiongeza kuwa ameweza kulipa fedha za pango ambazo alikuwa anadaiwa. 

Ijapokuwa Zahra ameweza kuondokana na tishio la kufukuzwa kwenye nyumba, hivi sasa yeye na wengine wengi bado wana hofu na uewzo wa kulipa pango. 

Hali ni hivyo hivyo kwa Hayat kutoka Syria, mjane mwenye umri wa miaka 50 anayeishi na watoto wake watatu  ambaye anasema, “ninalazimika kukopa fedha na kutegemea ukarimu wa watu ili niweze kulipa pango. Lakini mwenye nyumba wetu ni mtu mzuri na anatuvumilia.” 

 Hayat kama ilivyo kwa Zahra, alipokea msaada wa fedha kutoka UNHR na matamanio yake ni kununulia binti zake watatu chochote watakacho lakini kile awezacho sasa ni mahitaji ya msingi ya familia na si nguo mpya ambazo watoto wake hao wanalilia. 

Hata hivyo alipatiwa msaada wa fedha kwa ajili ya kulipia gharama za elimu kwa watoto wake wawili. 

Msaada huo unatolewa na UNHCR kupitia mdau wake Catholic Relief Services, kwa lengo la kuwezesha watoto wakimbizi kuendelea na elimu.