Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na wataalam wanataka hatua za haraka kuanza tena kwa huduma za chanjo Afrika.  

Watoto wakisubiri kuchanjwa dhidi ya polio kwenye mitaa ya Mogadishu nchini Somalia.
© UNICEF/Ismail Taxta
Watoto wakisubiri kuchanjwa dhidi ya polio kwenye mitaa ya Mogadishu nchini Somalia.

WHO na wataalam wanataka hatua za haraka kuanza tena kwa huduma za chanjo Afrika.  

Afya

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, WHO na kundi la wataalam washauri wa chanjo katika ukanda wa Afrika, RITAG,  wametoa wito kwa nchi na wadau wa afya kutanguliza huduma za chanjo ambazo zimevurugwa na janga la COVID-19 ili kulinda watoto na jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuiliwa na chanjo. 

Taarifa ya WHO iliyotolewa hii leo katika mji mkuu wa Jamhuri ya Congo, Brazzaville imesema wakati nchi zinajiandaa kwa chanjo za COVID-19, wataalam wanaonya kuwa kupungua kwa idadi ya wanaochanjwa dhidi ya magonjwa mengine, kunaweza kusababisha kuzuka kwa magonjwa mengine yanayoweza kuzuiwa kwa chanjo.   

RITAG ambao wamefanya mkutano kuanzia tarehe 18 hadi 19 ya mwezi huu wa Novemba ili kujadili hali ya chanjo katika ukanda wa Afrika na kujiandaa kwa ajili ya chanjo ya COVID-19 wamesema kuna haja ya kuwa na hatua za haraka kuanza tena kwa huduma za chanjo.   

Dkt. Matshindiso Moeti amabye ni Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika amesema, “COVID-19 imevuruga utoaji wa huduma muhimu za afya, pamoja na chanjo ya kawaida. Hii inaweka watu katika hatari ya magonjwa yanayoweza kuzuiliwa na chanjo na kutishia faida tuliyopata hadi sasa. Tunapojiandaa kwa chanjo ya COVID-19, lazima tuhakikishe kuwa chanjo za kuokoa maisha ambazo tayari tunazo zinawafikia wale walioko katika uhitaji zaidi.” 

Mnamo mwaka wa 2019, usambazaji wa chanjo katika eneo la Afrika ulidumaa katika asilimia 74 kwa dozi ya tatu ya chanjo ya diphtheria-tetanus-pertussis iliyo na chanjo ya DTP3, na katika asilimi 69 kwa dozi ya kwanza ya chanjo ya surua chini kabisa ya lengo la ukanda ambalo ni asilimia 90. Mapungufu haya katika chanjo yamezidishwa mnamo 2020 na janga la COVID-19, ikiweka mamilioni ya watoto katika hatari ya magonjwa hatari. 

Kwa mfano, watoto zaidi ya milioni 1.37 katika eneo lote la Afrika walikosa chanjo ya Bacille Calmette-Guerin (BCG) ambayo inawalinda dhidi ya Kifua Kikuu na watoto zaidi ya milioni 1.32 chini ya umri wa mwaka mmoja hawakupata dozi yao ya kwanza ya chanjo ya surua kati ya Januari na Agosti 2020, ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha mwaka 2019. Kampeni za chanjo zinazohusu ugonjwa wa surua, homa ya manjano, polio na magonjwa mengine yameahirishwa katika nchi 15 za Kiafrika mwaka huu. 

"Hatua za pamoja za kuimarisha chanjo zinahitajika, sasa zaidi ya hapo awali, tunapokaribia mwisho wa muongo wa chanjo na COVID-19 inapunguza upatikanaji wa huduma muhimu za afya kote Afrika," amesisitiza Profesa Helen Rees, Mwenyekiti wa RITAG. 

Wataalam waliohudhuria mkutano huo pia wamejadili hitaji la nchi kuweka msingi wa kuanzishwa na kutolewa kwa chanjo ya COVID-19, kama kipaumbele cha haraka. Wanachama wa RITAG wameisihi WHO na washirika wake,  kushirikisha wadau wote husika katika mchakato wa utayarishaji wa chanjo, pamoja na uongozi wa kitaifa.