Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hongera Maziwa Makuu kwa kudumisha ushirikiano na ujumuishwaji lakini msibweteke:UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres
UN News
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres

Hongera Maziwa Makuu kwa kudumisha ushirikiano na ujumuishwaji lakini msibweteke:UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezipongeza nchi za ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika kwa hatua kubwa walizofikia hivi karibuni katika kuboresha uhusiano kati ya nchi za Ukanda huo, kupambana na vikundi vyenye silaha na pia maendeleo katika suala la ujumuishaji, kukuza uchumi wa ukanda huo na haki za binadamu.

Antonio Guterres katika ujumbe wake wa video kwa mkutano huo wa 8 wa kimataifa wa kanda ya Maziwa Makuu unaofanyika kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao amesema katika zama hizi za janga la corona au COVID-19 ambalo halikuinusuru nchi yoyote duniani amesifu uimara wa ukanda huo na hatua zilizochukuliwa na serikali zao kuzuia kusambaa zaidi kwa janga hilo.

Ameongeza kuwa mkutano huo unampa fursa ya kuelezea mchango wa mkutano mkuu wa kimataifa kwa ajili ya kanda ya maziwa makuu katika kukuza amani na maendeleo endeleve katika ukanda huo.

‘Ukanda wa Maziwa Makuu unapaswa kujivunia maendeleo makubwa yaliyopatikana hadi sasa lakini amewaasa kwamba hawapaswi kubweteka na maendeleo hayo kwa sababu ya changamoto nyingi ambazo hivi sasa zinazidishwa na COVID-19. Shughuli za makundi yenye silaha pia zinasalia kuwa tishio kubwa kwa maisha ya ustawi wa raia wanaolazimika kuhama na kukimbia mara kwa mara. ’

Anurith, mkimbizi kutoka DRC akisaka hifadhi Uganda.
VIDEO YA UNHCR
Anurith, mkimbizi kutoka DRC akisaka hifadhi Uganda.

Usisitishaji uhasama

Guterres ameongeza kuwa hali ya kukokuwepo kwa usalama kunazuia shughuli za koiuchumi na misaada ya kibinadamu, kunadhoofisha utulivu wa ukanda huo na kuathiri juhudi za kuelekea maendeleo endelevu.

Kwa mantiki hiyo amesema‘Narejea wito wangu wa kusitisha mapigano kwa vikundi vyote vyenye silaha. Vita dhidi ya vikundi hivi haviwezi kumalizika kwa njia ya kijeshi hivyo ni muhimu kuharakisha utekelezaji wa hatua zisizo za kijeshi ambazo tayari zimebainishwa na nchi za ukanda huu.’

Amesema vikundi hivi vyenye silaha pia hufaidika na unyakuaji haramu wa maliasili, kwa hivyo usimamizi imara na wa uwazi wa rasilimali hizi kwa faida ya watu wa ukanda huu ni muhimu.

Na kuhusu suala la ugaidi Katimu mkuu amesema‘Ninapenda kuelezea mshikamano wangu wa watu na serikali za Ukanda wa Maziwa Makuu kuhusu kuibuka kwa tishio la ugaidi ambalo sio tu liaashiria hatari kwa eneo hilo lakini kwa bara hili na ulimwengu wote.’

Pia ameziasa nchi za ukanda huo kushiriki katika michakato ya kisiasa iliyo jumuishi, kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa namba 1325 linalohusu wanawake, amani na usalama.

MMwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukanda wa Maziwa Makuu, Huang Xia
UN News/Li Zhang
MMwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukanda wa Maziwa Makuu, Huang Xia

Mchakato wa uchaguzi

Bwana Guterres amesema katika kuelekea kwa chaguzi zilizopangwa kufanyika katika nchi za Ukanda huo amesema ‘Napenda kusisitiza umuhimu wa kuweka mazingira wezeshi ya kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia, amani na za kuaminika.’

Amesisitiza kwamba ushirikiano ulioboreshwa ni muhimu pia katika kuzuia na kupambana na ukiukaji wa haki za binadamu na kuwawajibisha wahusika, lakini pia kukabiliana na unyanyasi wa kijinsia.

Ameziahidi nchi za Ukanda huo kwamba mfumo wa Umoja wa Mataifa utaendelea kutoa msaada kamilifu kwa juhudi za amani, usalama na maendeleo katika nchi za Maziwa Makuu.

Amesema ni kwa mantiki hiyo ndio maana‘mkakati mpya wa ujumuishwaji wa amani, kuzuia na kutatua migogoro katika eneo la Maziwa Makuu ulianzishwa na mjumbe wangu maalum kwa ajili ya ukanda huu Huang Xia. Mkakati huu unachangia kikamilifu katika kutimiza ahadi zilizotolewa chini ya mkataba wa usalama, utulivu na maendeleo na pia mkataba wa mfumo wa amani, usalama na ushirikiano wa DRC na eneo hilo.’