Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko Burkina Faso kwa kuweka mazingira bora ya mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu Kesho:Guterres

Wakazi wa Kaya, Burkina Faso wakipokea mgao wa chakula.
WFP/Mahamady Ouedraogo
Wakazi wa Kaya, Burkina Faso wakipokea mgao wa chakula.

Heko Burkina Faso kwa kuweka mazingira bora ya mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu Kesho:Guterres

Amani na Usalama

Katika mkesha wa kuamkia uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge nchini Burkina Faso hapo kesho Jumapili Novemba 22, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameipongeza serikali, viongozi wa kisiasa na watu wa Burkina Faso kwa kudumisha mazingira ya kuheshimiana katika wakati wote wa mchakato wa uchaguzi licha ya changamoto lukuki zinazolikabili taifa hilo la Afrika Magharibi.

Katika ujumbe uliotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani, Antonio Guterres ametoa wito kwa wadau wote katika uchaguzi huo kuendeleza mazingira hayo na kuhakikisha kwamba uchaguzi wa kesho Jumapili unafanyika kwa njia ya amani, jumuishi na wa kuaminika.

Katibu Mkuu pia amevitaka vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kufanya kila juhudi kuwalinda raia nchi nzima wakati wakipiga kura kutekeleza haki yao ya demokrasia na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Guterres amerejea kusisitiza ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia juhudi za kitaifa za kuwa na utawala wa kidemokrasia, kuchagiza muungano wa kijamii na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu nchini Burkina Faso.

 Rais wa sasa aliyeko madarakani Roch Marc Christina Kabore anashiriki uchaguzi huo akisaka muhula wa pili wa miaka 5 huku akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Eddie Komboigo kiongozi wa chama cha upinzani cha Congress for Democracy and Progress (CDP) chama kilichokuwa cha rais wa zamani wan chi hiyo Blaise Compaore ambaye alitolewa madarakani na machafuko mashuhuri yaliyozuka nchini humo mwaka 2014.