Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wangu kwa G20 ni rahisi: Tunahitaji mshikamano na ushirikiano-Guterres 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari, New York.
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari, New York.

Ujumbe wangu kwa G20 ni rahisi: Tunahitaji mshikamano na ushirikiano-Guterres 

Afya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwahutubia wanahabari hii leo mjini New York Marekani, kuhusu mkutano wa kesho wa viongozi wa nchi 20 zilizo na uchumi mkubwa duniani, G20, ameanza kwa kueleza kuwa mkutano huu unakuja wakati ambao janga la COVID-19 linaendelea kuuharibu ulimwengu. 

Bwana Guterres ameeleza kuwa atashiriki mkutano huo na ujumbe wake mkuu ni rahisi, “tunahitaji mshikamano na ushirikiano.” Kisha akiongeza kuwa dunia inahitaji hatua madhubuti sasa hususani kwa watu waliko hatarini zaidi.  

Katibu Mkuu Guterres akieleza namna ya kufikia hayo anasema, “hasa, lazima tuendelee kwa namna mbili: Kwanza, kupona kwa njia ambayo ni shirikishi kuleta kila mtu pamoja. 

Pili, kupona kwa njia ambayo ni endelevu, ikimaanisha, juu ya yote, hatua za ziada dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. 

Aidha Bwana Guterres ameeleza kuwa mafanikio ya hivi karibuni kwenye chanjo za COVID-19 yanatoa mwangaza wa matumaini lakini, “mwanga huo wa matumaini unahitaji kufikia kila mtu.” 

Hiyo ikimaanisha kuhakikisha chanjo zinachukuliwa kama bidhaa ya jamii kimataifa, chanjo ya watu ambayo inapatikana na nafuu kwa kila mtu, kila mahali. Na kwamba hili si zoezi la "kufanya mema" bali ni njia pekee ya kuzuia janga.
 

“Mfumo wa ACT- Accelerator ulioandaliwa na WHO na wadau ili kuongeza kasi ya kutengeneza, kuzalisha na kuwezesha kupatikana kwa vipimo na chanjo dhidi ya COVID-19 pamoja na COVAX wa kushughulikia chanjo ndiyo chombo cha kutufikisha tunakotaka kufika” Ameeleza Guterres akiongeza kuwa  katika kipindi cha miezi saba iliyopita, nchi zimewekeza dola bilioni 10 katika juhudi za kupata chanjo, uchunguzi na tiba. Lakini dola bilioni 28 zaidi zinahitajika - pamoja na $ 4.2 bilioni kabla ya mwisho wa mwaka. 

Bwana Guterres ameeleza kuwa nchi za G20 zina rasilimali na kwa hivyo anazisihi kutoa ufadhili zaidi kwani ni muhimu kwa uzalishaji, ununuzi na usambazaji wa chanjo ya COVID-19 duniani kote.