Kutoka Libya hadi Rwanda, wahamiaji waeleza matumaini mapya 

20 Novemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesafirisha kundi la wahamiaji 79 kutoka Libya kwenda Rwanda, ikiwa ni sehemu ya kuhamisha wahamiaji walio hatarini zaidi kwenda maeneo salama. 

UNHCR imesema kuwa hatua hiyo muhimu ilikuwa imekwama kwa takribani mwaka mzima kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 lililosababisha kufungwa kwa mipaka na hata vizuizi vya kutembea. 

Idadi hiyo ya wahamiaji waliosafirishwa Alhamisi kwenda Rwanda inafanya idadi ya watu wote waliosafirishwa kupitia mpango wa usafirishaji wa dharura, ETM wa serikali ya Rwanda, UNHCR na Muungano wa Afrika, AU uliotiwa saini mwaka 2019 kufikia 306. 

Ndege iliyokodishwa na UNHCR iliondoka mji mkuu wa Libya alhamisi mchana na kutua salama kwenye uwanja wa ndege wa Kigali nchini Rwanda ambapo wahamiaji ni pamoja na wanawake, wanaume na watoto kutoka Eritrea, Sudan na Somalia.  

Wengi wao walikuwa wanaishi Tripoli, lakini wengine pia walikuwa wamewekwa korokoroni kwa miaka kadhaa kwenye mji mkuu huo wa Libya. 

Abrahet, kutoka Eritrea anasema amekuwepo kwenye bohari huko Bani Walid baada ya kunusurika kifo. “nashukuru Mungu kwamba nimeweza kufika hapa na sasa nina matumaini na mustakabali wangu. Natumai maisha yangu yatakuwa mazuri baadaye. Nimepitia magumu mengi Libya. Nimenusurika kifo baharini na jangwani. Mungu amenisaidia nimefika hapa. Natumai watu tuliowaacha nyuma watakuwa na amani kama mimi. Natumai kufika kule ambako watu wetu wanaishi. Sasa hivi hakuna tena kikwazo cha furaha kwangu.” 

UNHCR hivi sasa inatoa wito kwa mataifa mengi zaidi kujitokeza kuchukua wasaka hifadhi walio hatarini kwa kuwa iwapo hakuna njia salama za uhamaji, watu wanaohaha kunusuru maisha yao wataendelea kufanya safari za hatari. 

Tsega, ambaye pia ni msaka hifadhi kutoka Eritrea anakiri kuwa wamekumbwa na machungu mengi. “Kuna wanawake na wanaume wengi wanaoishi kwenye bohari. Kwenye kituo cha kuweka watu ndani cha Tirik Sikka, kuna wanaume ambao wamewekwa ndani hata hawafahamu ni lini wataona mwanga lakini bado wana machungu. Kuna wanawake ambao angalau wanatoka nje lakini bado wana machungu. 

Wito wa Tsega kwa serikali duniani kote ni kusaidia watu wanaokumbwa na machungu Libya akisema matatizo wanayokumbana nayo si njaa peke yake, bali pia kuna kutekwa nyara, kuuzwa na hata kununuliwa. 

Wasaka hifadhi nchini Libya ambao wanahamishwa Rwanda wamepatiwa hifadhi katika kituo cha Gashora ambako UNHCR inawapatia misaada muhimu ikiwemo malazi, chakula, maji, dawa na msaada wa kisaikolojia na mafunzo ya lugha. 

Wasaka hifadhi hao watakuwepo kwenye kituo hicho wakati suluhisho zikisakwa kama vile malazi, kurejea nyumbani kwao kwa hiari kama kuna usalama au kujumuishwa kwenye jamii za Kinyarwanda. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter