Ingawa tunalazimika kuvaa barakoa lakini hatupaswi kufungwa midomo:Watoto

20 Novemba 2020

Leo ni siku ya watoto duniani maudhui yakiwa "kutafakari dunia bora kwa kila mtoto", na watoto kutoka kila kona ya dunia kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, wameandika shairi kufikisha ujumbe muhimu kwa viongozi wa dunia hii, wazazi na jamii wakitaka sauti zao zisikike na hatua zichukuliwe kulinda kizazi hiki na vijavyo.

Hiyo ni sehemu ya shairi hilo lililoandikwa na watoto kutoka mabara yote ya dunia wakisema wanafahamu madhila yanayoikumba dunia nje ya madirisha ya nyumba zao, kuanzia janga la corona au COVID-19 ambalo limesababisha hospitali kufurika na uchungu mkubwa kila kona janga ambalo hata wao halikuwanusuru. 

Ujumbe wao unaendelea kuumulika majanga mengine,“Tunasikia kilio cha mama dunia na sisi ni watoto wake hamuwezi kutunyamazisha, kwani dunia itasikia shairi letu kwa ajili ya misitu yake, na wimbo wetu kwa ajili ya bahari zake, kwa pamoja wito wetu utakuwa ni ngurumo”. 

Katika shairi lao lililohaririwa na kuchapishwa na UNICEF lwatoto wameweka bayana kwamba wao si wadogo sana kushindwa kutambua masuala yanayowaathiri kama mabadiliko ya tabianchi, ubaguzi, ubaguzi wa rangi na kutokuwepo kwa usawa na sasa wanachokitaka ni hatua kuchukuliwa ili kukomesha chagamoto hizo wawe na mustakbali bora.“Tumevaa barakoa lakini hatujazibwa midomo, mimi na wewe, kwa pamoja tutautafakari ulimwengu huu kwa sababu hii ndio njia yetu, hii ni dunia yetu na hii ni siku yetu.” 

Wakihitisha shairi lao wanasema siku zote mtoto anapaswa kuwa mtoto na huu ni wakati wa dunia kufungua macho kuyaona, kuyasikia na kuyafanyiakazi yanayomsibu mtoto huyu na si kumnyamazisha .

Ni ujumbe mahsusi ambao bilashaka  umewafikia walengwa.Siku ya watoto duniani huadhimishwa kila mwaka Novemba 20. 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter