Tunahofia kushindwa kufikisha msaada kwa maelfu ya wanaouhitaji Tigray Ethiopia:WFP/UNICEF 

Wakimbizi wa Ethiopia wanaokimbia machafuko kutoka kwa eneo la Tigray wakivuka mto wa Tekeze na kuingia Hamdayet, Sudan
© UNHCR/Hazim Elhag
Wakimbizi wa Ethiopia wanaokimbia machafuko kutoka kwa eneo la Tigray wakivuka mto wa Tekeze na kuingia Hamdayet, Sudan

Tunahofia kushindwa kufikisha msaada kwa maelfu ya wanaouhitaji Tigray Ethiopia:WFP/UNICEF 

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la mpango wa chakula duniani WFP na la kuhudumia Watoto UNICEF, leo yameelezea hofu yake ya kushindwa kuwafikia wakimbizi 100,000 wakiwemo watoto katika jimbo la Tigray Ethiopia kwa misaada muhimu ya kuokoa maisha ikiwemo chanjo na elimu.

Katika jimbo hilo la Tigray Kaskazini mwa Ethiopia ambako mapigano yanaendelea baina ya vikosi vya ulinzi vya serikali kuu na jeshi la ukombozi la watu wa Tigray mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yanasema imekuwa vigumu kuwafikia watu wanaohitaji msaada kwani mawasiliano yamekatwa na njia zote za usafiri zimevurugwa ndani nan je ya jimbo hilo na hivyo kushindwa kupata njia yoyote ya kufikisha chakula, huduma za afya na mahitaji mengine kama vifaa vya malazi na hata kufuatilia masuala kama ya chanjo kwa watoto au upatikajani wa elimu.  

Jimbo la Tigray limekuwa likihifadhi makundi mbalimbali ya watu walio hatarini ikiwa ni Pamoja na watu 855,000 wanaopatiwa msaada wa kibinadamu, wakimbizi 96,000 kutoka Eritrea na watu wengine zaidi ya milioni moja wasiojiweza wakiwemo watoto ambao wako kwenye program za misaada za Umoja wa Mataifa na sasa kuna maelfu ya wakimbizi wapya wa ndani na na wanaokimbilia nchi jirani ya Sudan ambao wengi ni watoto. Fadula Abdul ni msemaji wa UNICEF mjini Khartoum Sudan,“Kitu cha kwanza tulichobaini ni kwamba karibu aslimia 45 ya wakimbizi ni watoto wa umri wa chini ya miaka 18. Kitu cha pili ni kuwa watu wamekimbia bila chochote, ingawa kuna walioondoka na wanyama wao, vitu kidogo na mavuno kidogo lakini wengi wamekimbia bila chochote na shule kwa watoto hawa zimevurugwa. Kwa sasa tunajipanga kwa msaada wa ongezeko la wakimbizi hadi 200,000 na hofu yetu kubwa ni kuwa endapo hatutochukua hatua haraka sasa kupata  rasilimali zinazohitajika hali itakuwa janga sio tu kwa Ethiopia lakini pia kwa Sudan.” 

WFP inasema hali ya kibinadamu inaendelea kuwa mbaya kwenye mpaka wa Ethiopia na Sudan ambako watu wanaokimbia jimbo la Tigray wanawasili na idadi inaongezeka kila uchao. Hivyo wamesema dola milioni 10  zinahitajika haraka kukidhi mahitaji ya chakula kwa wakimbizi hao wanaoendelea kuwasili. 

Hadi sasa fedha zilizopatikana n idola milioni 5 zilizotolewa na ufalme wa nchi za Kiarabu UAE ambazo zitasaidia kulisha wakimbizi 53,000 kwa kipindi cha miezi sita.