Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilianza kufanya kazi nikiwa darasa la pili, siku nzima nililala kwa saa moja-Mtoto Ko Ko Kyaw 

Mvulana Ko Ko Kyaw ambaye amekuwa akifanya kazi tangu alipokuwa na umri wa miaka 7 nchini Myanmar.
ILO/Video Capture
Mvulana Ko Ko Kyaw ambaye amekuwa akifanya kazi tangu alipokuwa na umri wa miaka 7 nchini Myanmar.

Nilianza kufanya kazi nikiwa darasa la pili, siku nzima nililala kwa saa moja-Mtoto Ko Ko Kyaw 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Filamu ya maisha halisi iliyotengenezwa na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa ILO kwa kushirikiana na kampuni ya PhotoDoc Association ya nchini Mynmar, imeonesha madhila mazito wanayoyapata watoto wanapotumikishwa katika ajira katika umri mdogo.

Ko Ko Kyaw, ni kijana mdogo, katika filamu kwa jina Burning Hands au mikono inayowaka moto ambayo inaeleza maisha yake halisi na watoto wenzake nchini Myanmar.  Ko Ko amekuwa akifanya kazi tangu akiwa na umri wa miaka saba, akibeba saruji kwenye maeneo ya ujenzi kwenye jua kali la Mandalay.  

Ko Ko anasema alianza kufanya kazi akiwa katika darasa la pili. Kazi yake ikiwa ni kujaza saruji katika makarai ya wajenzi. 

Alipoongezeka umri kidogo, wakaanza kumwongezea kazi ngumu za kuchosha zaidi. 

Anasema, katika mazingira yao magumu unapofikia umri wa miaka 10, wewe si mtoto tena. Anaongeza kusema kuwa kuna vitu vyeupe na vyeusi ambavyo huchanganywa kwenye saruji ili jengo liwe imara, kwa hivyo wanapobeba makarai, mikono yao inaungua na wakati mwingine inavuja damu.  

Anaeleza kuwa alipokuwa na umri wa miaka 11 yeye pamoja na marafiki zake wawili walienda kufanya kazi na watu wengine wazima 40, saa tatu kutoka Mandalay. Walilazimika kufanya kazi siku nzima isipokuwa saa moja tu la kupata japo lepe la usingizi. Mtoto Ko Ko anasema baada ya kazi miguu inauma, nyayo zinavuja damu huwezi hata kwenda kuoga, na hata chakula walichopewa walikuwa wanashindwa kukigusa kwani mikono inavuja damu. Nilitaka kulia, anasema. 

Ko Ko ana ndoto ya maisha bora ya baadaye kwake na dada zake, ambao pia wako katika ajira za watoto. Anataka maisha yenye kuchora, kujifunza na kutoroka mateso ya mwili. Lakini ugonjwa wa COVID-19 nao umeifanya ndoto hii sasa inaonekana kuwa mbali zaidi. 

Anasema mara ya kwanza alisikia kuhusu ugonjwa huu kutoka kwa marafiki zake. Walimweleza kuwa hawataweza kufanya kazi kwa muda kutokana na COVID-19, anajiuliza, wanapata chakula wanapolipwa, sasa kutokana na ugonjwa huu wa virusi vya corona, watakula vipi? 

Mnamo mwezi Juni mwaka 2020, Myanmar iliridhia mkataba mpya wa kimataifa wa wafanyakazi ambao unakataza watoto wa umri wa miaka 14 na chini kufanya kazi, na wote walio chini ya miaka 18 wasifanye kazi katika mazingira hatarishi. Sasa ni wakati wa kubadili sera kuwa vitendo. Wakati wa kumaliza hadithi kama hii ya Ko Ko.