Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ninaumia kwa kinachoendelea nyumbani Ethiopia siwezi kuegemea upande wowote:Dkt.Tedros 

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza katika moja ya taarifa za WHO kuhusu janga la COVID-19
UN Photo/Evan Schneider
Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza katika moja ya taarifa za WHO kuhusu janga la COVID-19

Ninaumia kwa kinachoendelea nyumbani Ethiopia siwezi kuegemea upande wowote:Dkt.Tedros 

Amani na Usalama

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema anaumia na kupata uchungu mkubwa moyoni kufuatia hali ya machafuko inayoendelea Ethiopia nchi anakotoka ,na amertoa wito kwa pande zote katika mzozo kufanya kila liwezikanalo kwa ajili ya kurejesha amani na kuhakikisha ulinzi wa raia na pia kutoa fursa za huduma za afya na misaada ya kibinadamu kwa wale wanao ihitaji. 

Katika taarifa yake fupi aliyoitoa leo kupitia ukurasa wake wa Twitter Dkt. Tedros ameandika “Nimeshtushwa san ana ripoti za vifo na majeruhi na idadi kubwa ya watu waliotawanywa na kuomba hifadhi katika nchi za jirani. Na ikiwa ni katikati ya janga la corona au COVID-19 hofu yangu inaongezeka kuhusu athari za kiafya.” 

Taarifa ya mkuu huyo wa WHO imekuja kufuatia ripoti katika vyombo vya Habari zinazodai kwamba anadegemea upande mmoja katika machafuko hayo yanayohusisha serikali ya Ethiopia na vikosi vya jimbo la Tigray la nchi hiyo , mzozo ulioibuka wiki iliyopita.  

Akikanusha ripoti hizo Dkt. Tedros amesema “Kuna ripoti zinazopendekeza kwamba mimi niegemea upande mmoja katika hali hiyo. Hii si kweli na nataka kusema kwamba niko katika upande mmoja pekee na upande huo ni wa amani. Dunia nzima inahitaji amani kwa ajili ya afya na afya kwa ajili ya amani.” 

Ameongeza kuwa “Nikiwa mtoto nimeshuhudia uharibifu unaoletwa na vita, nakumbuka bayana mapigano na athari zake mbaya kwa binadamu. Na nilipokuwa mtu mzima nimekuwa nikitumia uzoefu kila wakati kupigania amani, kuzileta Pamoja pande kinzani na kuanzisha majadiliano ili kuleta amani.” 

Amesisitiza kwamba historia inakuwa nzuri kwa wale wanaoweza kuvuka upande wa pili, wanaoweza kuondoa migawanyiko na wanaoweza kutoka kwenye vita na kuingia kwenye amani. 

“Naungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kuchukua hatua za haraka kusitisha mvutano na kuhakikisha suluhu ya amani ya mzozo huo.” 

TAGS:WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, Ethiopia, machafuko