Skip to main content

Makazi ya ulinzi wa raia yameanza kuwa makazi ya wakimbizi wa ndani Sudan Kusini:UNMISS 

Mapigano ya kikabilia yameathiri jamii Pibor mashariki mwa Sudan Kusini.
UN Photo/Isaac Billy
Mapigano ya kikabilia yameathiri jamii Pibor mashariki mwa Sudan Kusini.

Makazi ya ulinzi wa raia yameanza kuwa makazi ya wakimbizi wa ndani Sudan Kusini:UNMISS 

Wahamiaji na Wakimbizi

Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umeshaanza rasmi kuyageuza makazi ya ulinzi wa raia (POCs) na kuwa makambi ya kawaida ya wakimbizi wa ndani kama ulivyoahidi.

Mjini Juba kwenye moja ya makazi ya Umoja wa Mataifa yaliyokuwa ya ulinzi wa raia pilikapilika ni nyingi kwani sasa yamegeuzwa rasmi na kuwa kambi ya wakimbizi wa ndani. Maelfu ya watu waliotawanywa na vita iliyozuka nchini humo mwaka 2013 walikimbilia katika makazi hayo kusaka usalama chini ya ulinzi wa UNMISS.

Sasa miaka saba baadaye hali imebadilika kwani machafuko yamepungua, uhasama umesitishwa kwa kiasi kikubwa, mkataba wa amani umetiwa saini na serikali ya umoja wa kitaifa imeundwa, hatua iliyofanya UNMISS kuanza kubadili makazi hayo ya ulinzi wa raia na kuwa makambi ya kawaida ya wakimbizi wa ndani na kuwa chini ya udhibiti wa serikali ya Sudan Kusini.

Na mambo yanakwenda shwari kama anavyosema mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa UNMISS nchini humo David Shearer,“Nina furahi kuarifu kwamba hadi sasa mchakato huu unaendelea bila dosari, jamii za wakimbizi wa ndani zimeyapokea vizuri mabadili haya licha ya hofu iliyokuwepo hapo mwanzo, na sasa wanashirikiana na mamlaka za eneo hili na polisi wa Sudan Kusini wanaosaidiwa na UNPOL na kwa msaada unaoendelea kutolewa na wahudumu wa kibinadamu.”

Wakimbizi hawa wa ndani wana uhuru mkubwa hivi sasa wa kutoka katika kambi moja hadi nyingine na pia kwenda mjini kufanyakazi, madukani na shuleni, na wanasema kinachowafanya kusalia katika makambi haya ni kupata msaada wa kibinadamu kuliko hofu za usalama.

Ukiacha hapa Juba makazi mengine ya ulinzi wa raia yaliyogeuzwa kuwa makambi ya wakimbizi wa ndani ni Wau na Born na Bwana Shearear anasema serikali ya Sudan Kusini ndio yenye wajibu mkubwa wa kuangalia makambi haya kama ilivyo kwa makambi mengine ya wakimbizi wa ndani nchini nzima.

Hata hivyo vikosi vya UNMISS na wafanyakazi wa kiraia watashirikiana na mamlaka za kijamii kuzuia machafuko, kuchagiza maridhiano na kujenga amani katika makambi haya ili familia ziweze kupata fursa ya kujijenga upya.