Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Niliona Kijiji chetu kina watu wawili tu waliosoma, nikaingia kwenye migodi kutafuta pesa-Lawrence  

Picha ya maktaba ikionesha wachimba dhahabu nchini Ghana.
Picha: IRIN/John Appiah
Picha ya maktaba ikionesha wachimba dhahabu nchini Ghana.

Niliona Kijiji chetu kina watu wawili tu waliosoma, nikaingia kwenye migodi kutafuta pesa-Lawrence  

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linaendelea kushirikiana na Serikali ya Uganda, sekta binafsi na washirika wengine kuhamasisha makampuni na wadau wote kuhusu haki za watoto na pia katika shughuli zao za kila siku, kuwa na sera rafiki za watoto. Hiyo ni kutokana na watoto wengi kutumikishwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi badala ya kuwa shuleni kama anavyoeleza mtoto Lawrence katika taarifa hii inayosimuliwa na Anold Kayanda. 

Lawrence, anaeleza kuwa alianza shughuli za uchimbaji madini akiwa mwanafusi wa shule ya msingi katika darasa la pili.  

Lawrence mwenye umri wa miaka 16 hivi sasa, alianza kufanya kazi katika mgodi wa dhahabu akiwa na umri wa miaka 6, kama msaidizi, akibeba vifusi na kuponda mawe. Alilazimika kusaidia baada ya baba yake kuugua. Alitaka apate pesa za kwenda shuleni ili awe na maisha bora ya baadaye lakini mambo hayakuwa marahisi mgodini. Hivi sasa anahudhuria katika Kituo cha hamasa cha Tiira na anaeleza hadithi ya maisha yake.   

Lawrence anasema aliona kijijini kwao kulikuwa na watu wawili waliosoma. Akaona ni muhimu na yeye apate elimu lakini hakuwa na usaidizi wowote na hapo ndipo marafiki zake wakamfundisha uchimbaji madini. 

Anasema huko unalipwa lakini kiasi ni kidogo na kazi ni ngumu. Unapewa kama beseni moja la mawe uyapondeponde na unaambulia shilingi elfu mbili ya Uganda ambayo ni chini ya dola moja ya kimarekani.  

Kituo cha Tiira kilichoko wilaya ya Busia, Mashariki mwa Uganda, kinajihusisha kuwahamasisha na kuwapa watoto motisha ya elimu, kilimchukua Lawrence na sasa ameachana na shughuli za migodi. Deo Mugeni ni mwalimu katika kituo hicho anasema, “tulipoongea naye tulimwambia, Lawrence, ndio unatafuta maisha, lakini bado wewe ni mtoto. Kazi unayoifanya itauathiri mwili wako. Kwa hivyo ilikuwa kiasi vigumu kwake kuacha lakini tuliongea naye hadi tulipomuahidi aje atembelee kituo chetu. Kwa hivyo alipokuja hapa tulimwelezea zaidi hasa kwa upande wa mwogozo wa kazi, uchimbaji madini utaisha Tiira, utakuwa wapi? Lawrence alielewa na akawa na sisi.” 

Mwalimu Mugeni anasema wazazi wa Lawrence waliupokea uamuzi huo ingawa kwa kiasi fulani lilikuwa pigo kwao kwani alikuwa anawaletea kipato kiasi. Kutokana na hamasa na ushauri unaotolewa na UNICEF kwa makampuni kuweka mazingira mazuri ya kusaidia elimu na ujuzi kwa watoto na vijana, bila shaka mstakabali wa Lawrence na wenzake, una matumaini.