Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC, Nigeria, Sudan Kusini na Burkina Faso miongoni mwa watakaonufaika na dola milioni 100 za UN 

Wanawake huko Ganyiel jimbo la Unity nchini Sudan Kusini wakisubiri mgao wa chakula. Hali ni mbaya ya chakula.
OCHA/Gemma Connell
Wanawake huko Ganyiel jimbo la Unity nchini Sudan Kusini wakisubiri mgao wa chakula. Hali ni mbaya ya chakula.

DRC, Nigeria, Sudan Kusini na Burkina Faso miongoni mwa watakaonufaika na dola milioni 100 za UN 

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya dharura, OCHA, Mark Lowcock leo ametengaza kuwa mfumo mkuu wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF umetenga na kuziachia dola milioni 100 za Kimarekani kusaidia watu kuweza kujipatia chakula wao wenyewe katika nchi zilizo hatarini zaidi kutokana na janga la njaa linalozidi kusababishwa na mizozo, kuporomoka kwa uchumi, mabadiliko ya hali ya hewa na janga la COVID-19. 

Afghanistan, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, Nigeria, Sudan Kusini na Yemen kila moja itapokea kiasi cha sehemu ya dola milioni 80 kutoka katika mfuko wa dharura wa UN (CERF). Dola za ziada milioni 20 zimetengwa kwa hatua ya kutarajia kupambana na njaa nchini Ethiopia, ambapo ukame unaweza kuzidisha hali dhaifu tayari. 

Fedha hizo zimetolewa pamoja na onyo kwamba bila hatua ya haraka, njaa inaweza kuwa kweli katika miezi ijayo katika sehemu za Burkina Faso, Kaskazini-mashariki mwa Nigeria, Sudan Kusini na Yemen. Hii itakuwa mara ya kwanza kutangazwa njaa tangu 2017 katika sehemu za Sudan Kusini. 

Mark Lowcock amesema, "matarajio ya kurudi kwenye ulimwengu ambao njaa ni kawaida itakuwa maumivu ya moyo na ya aibu katika ulimwengu ambao kuna chakula cha kutosha kwa kila mtu." 

Bwana Lowcock ameongeza akisema, “njaa husababisha vifo vya kuumiza na kudhalilisha. Vinachochea migogoro na vita. Vinasababisha ufurushaji wa watu wengi. Athari zake kwa nchi ni mbaya na hudumu kwa muda mrefu. Hakuna mtu anayepaswa kutazama kuingia katika njaa kama athari ya isiyoepukika ya janga hili. Ikitokea ni kwa sababu ulimwengu umeruhusu iweze kutokea. Njaa inaweza kuzuiwa. Lakini lazima tuchukue hatua kwa wakati ili kuleta mabadiliko. Hivi sasa, pesa zaidi kwa shughuli ya misaada ndio njia ya haraka na bora zaidi ya kuunga mkono juhudi za kuzuia njaa. " 

“Pesa taslimu kutoka CERF yaani dola milioni 80 itasambazwa kupitia programu ya pesa taslimu na vocha, moja wapo ya njia bora zaidi, rahisi na ya gharama nafuu kusaidia watu wenye uhitaji mkubwa sana.” Imeeleza taarifa ya OCHA.  

Afghanistan, ambapo watu milioni 3.3 wanakabiliwa na kiwango cha dharura cha uhaba wa chakula ikimaanisha kuwa wako hatua moja kutoka baa la njaa watapokea dola milioni 15. 

Burkina Faso itapokea dola milioni 6. Idadi ya watu wenye njaa kali nchini humo karibu imeongezeka mara tatu tangu 2019, na zaidi ya watu 11,000 tayari wako katika hali mbaya. 

DRC itapokea dola milioni 7.  Kaskazini Mashariki mwa Nigeria watapokea dola milioni 15. Maeneo yanayotia wasiwasi katika Nigeria ni yale yaliyoathirika na mgogoro hususani sehemu za jimbo la Borno ambako misaada ya kibinadamu ni vigumu kufika.  

Sudan Kusini itapata dola milioni 7. Robo ya wakazi wa Jimbo la Jonglei walitarajiwa kufikia ukingo wa njaa ifikapo Julai 2020. 

Yemen itapokea dola milioni 30 kusaidia kulisha mamilioni ya watu ambao wamesukumwa kwenye makali ya njaa na miaka mitano ya vita. 

 “CERF ni moja wapo ya njia ya haraka zaidi na bora ya kusaidia watu walioathiriwa na mizozo. Tangu ilipoanzishwa mnamo 2005, mfuko huo umetoa karibu dola bilioni 7 kwa hatua ya kuokoa maisha ambayo imesaidia mamilioni ya watu katika nchi na wilaya zaidi ya 100. Hii isingewezekana bila msaada wa wafadhili wenye ukarimu na thabiti.” Imesema OCHA