Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu wazidi kukimbia Cabo Delgado, usaidizi wakumbwa na mkwamo 

Wafanyakazi wa IOM wakiwa na wakimbizi wa ndani katika jimbo la Cabo Delgado.
UN Mozambique/Helvisney Cardosordoso
Wafanyakazi wa IOM wakiwa na wakimbizi wa ndani katika jimbo la Cabo Delgado.

Maelfu wazidi kukimbia Cabo Delgado, usaidizi wakumbwa na mkwamo 

Amani na Usalama

Makumi ya maelfu ya wananchi wanaendelea kukimbia ghasia jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji huku serikali na wadau wa kibinadamu wakishindwa kukidhi mahitaji ya watu hao ya malazi, chakula na misaada mingine.

Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM limesema takwimu mpya za zinaonesha kuwa wanaokimbilia kusini mwa nchi hiyo idadi imeongezeka mara nne kutoka 88,000 mapema mwaka huu hadi zaidi ya 355,000 hivi sasa. 

Taarifa ya IOM iliyotolewa leo huko Pemba, Cabo Delgado nchini Msumbiji imenukuu wakimbizi hao wakisimulia yale waliyopitia ambapo mmoja wao ameiambia IOM “pindi mashambulio yalipotokea, kijiji chetu Macomia kilitiwa moto wakati tukiwa shambani.” 

Mkimbizi huyo Salimo Nvita mwenye familia ya watu 7 wazima na watoto 11 amesema walikimbia na nguo tu walizokuwa wamevalia na kwamba wamepoteza kila kitu. Hivi sasa Salimo na familia yake wanapokea msaada kutoka IOM. 

Mkuu wa IOM nchini Msumbiji Laura Tomm-Bonde amesema hivi sasa wanapatia maelfu ya familia misaada kwa kushirikiana na serikali ya Msumbiji. 

“Hata hivyo rasilimali tulizonazo haziwezi kutosheleza mahitaji ya watu hao wanaowasili bila kitu chochote baada ya kukimbia makazi yao,” amesema Bi. Tom-Bonde. 

Ukosefu wa usalama umezuia IOM kufikia wilaya kadhaa za kaskazini na ukanda wa pwani mwa Cabo Delgado, ingawa hivyo wafanyakazi wa IOM baad iyao wameendelea kusaidia wakimbizi katika wilaya zingine 8 ambako wanaweza kutoa huduma. 

Tangu tarehe 16 mwezi Oktoba hadi tarehe 14 mwezi huu wa Novemba, wakimbizi 14,400 wamewasili kwa boti katika pwani ya Paquitequete ya mjini Pemba huko Cabo Delgado ambapo kwa sasa kila siku boti 29 zinawasili zikiwa na wakimbizi. 

Mahitaji ya dharura hivi sasa ni malazi, ulinzi na usaidizi wa kisaikolojia pamoja na chakula na huduma za kujisafi. 

Wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alielezea wasiwasi wake juu ya janga linaloendelea huko Cabo Delgado ikiwemo watu waliojihami kuua wananchi kwa kuwakata vichwa na hata kubaka wanawake na watoto, na hivyo kutoa wito wa kutaka mzozo huo kati ya serikali na vikundi vilivyojihami vichukue hatua.