Licha ya COVID-19, vita dhidi ya ugaidi Sahel imeendelea vema lakini ushirikiano zaidi unahitajika-Lacroix 

Wakimbizi wa ndani (IDPs) katika kijiji kwenye eneo la Mopti la Mali.
MINUSMA/Marco Dormino.
Wakimbizi wa ndani (IDPs) katika kijiji kwenye eneo la Mopti la Mali.

Licha ya COVID-19, vita dhidi ya ugaidi Sahel imeendelea vema lakini ushirikiano zaidi unahitajika-Lacroix 

Amani na Usalama

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo  kuhusu amani na usalama barani Afrika amesema tangu mjadala wa Baraza la Usalama lilofanyika mnamo tarehe 5 Juni mwaka huu kuhusu Sahel, vita dhidi ya ugaidi katika eneo la Sahel imeendelea kuhamasishwa katika ngazi ya kikanda, bara na kimataifa licha ya muktadha unaoendelea wa janga la COVID-19 na pia kwamba ushirikiano zaidi unahitajika.  

“Inachukua wahusika tofautitofauti kukabiliana na changamoto za kutisha katika ukanda huo, na katika suala hili, tunakaribisha ongezeko la uratibu wa wanausalama katika eneo. Uratibu huu wa juhudi uliruhusu uwepo dhahiri wa vikosi vya ulinzi na usalama katika ukanda huo na pia kuzidisha shinikizo kwa vikundi vya kigaidi.” Amesema Lacroix.  

Aidha Bwana Lacroix ameongeza kusema, “pamoja na janga la COVID-19, ni muhimu kuzingatia kwamba juhudi za kupambana na ugaidi huko Sahel zimeongezeka. Kutokana na hali hii, Kikosi cha Pamoja kinabaki kuwa sehemu muhimu ya majibu ya usalama kushughulikia vikundi vyenye silaha kali katika ukanda huo, pamoja na changamoto zingine za nje ya mpaka, pamoja na usafirishaji haramu wa watu, bidhaa haramu, silaha na dawa za kulevya.” 

Lacrox amesema tangu ripoti ya mwisho ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kikosi cha pamoja cha nchi tano za Sahel kutoka Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara, G5 kimeendelea kukua katika nguvu zake za operesheni. Vitengo vya Kikosi cha pamoja vimezidi kupata uzoefu na ufanisi katika utendaji wao. Operesheni Sama 1 ilimalizika tarehe 31 Julai na ilipimwa vyema, ikiwa imesababisha hasara kubwa kwa uapnde wa vikundi vya kigaidi. Operesheni Sama 2, iliyozinduliwa mnamo 1 Agosti, inatarajiwa kudumu hadi mwisho wa Januari 2021, kukiwa na matumaini chanya na makubwa.  

Zaidi ya idhini ya Baraza la Usalama kwa MINUSMA kushirikisha makandarasi wa kibiashara kuleta vifaa vya msaada wa maisha kwa vikosi vya pamoja vinavyofanya kazi nje ya eneo la Mali, Bwana Lacrox amesema ujumbe ulianza kufanya mipango inayofaa kutekeleza msaada huo. “Kulingana na mahitaji yaliyotambuliwa na kukubaliwa na G5 Sahel, MINUSMA sasa inaweza kuendeleza mchakato wa ununuzi. Hata hivyo, kama ilivyoainishwa katika ripoti mfululizo za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, upungufu wa mtindo wa sasa wa msaada unaonesha vizuizi muhimu.” 

Suala la ufadhili wa fedha unaotabirika bado ni la kutia wasiwasi. 

Umoja wa Mataifa, pamoja na G5 Sahel na washirika wengine, wanaendelea kutoa wito kwa ufadhili unaotabirika zaidi. Kikosi cha Pamoja cha G5 Sahel kina jukumu muhimu katika kushughulikia suala la eneo la Sahel. Katika suala hili, ni muhimu kwamba ipokee misaada inayohitajika kutekeleza majukumu yake yaliyoamriwa.” Amesema Bwana Lacroix 

Kwa mujibu wa Lacrox, kutokana na ombi la Baraza la Usalama, Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa itafanya tathmini ya msaada wa MINUSMA kwa Kikosi cha pamoja chini ya azimio la 2531 (2020) mapema 2021. Tathmini hii haitaonyesha tu maendeleo yaliyopatikana katika suala hili, lakini pia changamoto katika kutekeleza mamlaka ya msaada ulioimarishwa. Hitimisho na mapendekezo ya tathmini hii yatazingatiwa katika ripoti ya robo mwaka ya pili ya 2021 ya Katibu Mkuu kuhusu  MINUSMA.