Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano ndio jawabu pekee la kukabili changamoto za dunia hivi sasa:Guterres 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari, New York.
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari, New York.

Ushirikiano ndio jawabu pekee la kukabili changamoto za dunia hivi sasa:Guterres 

Masuala ya UM

Janga la corona au COVID-19 linabadili hatua zilizopigwa katika maendeleo na kuujaribu msingi wa amani ya kimataifa, lakini pia linatoa fiursa ya kushirikiana kuzisaidia serikali na jamii kujijenga vyema upya  umesema mkutano wa kimataifa ulioanza leo kwa njia ya mtandao mjini Roma Italia ukiwaleta pamoja wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, taasisi za fedha za kimataifa, Muungano wa Afrika naserikali za Muungano wa Ulaya.

Akizungumza katika mkutano huo kabla ya majadiliano na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel  wa mwaka 2020 ,shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Wakati nchi zikijijenga upya na kufufua uchumi ni lazima tuongeze kasi ya kuingia katika nishati jadidifu, tubadili mwelekeo katika mifumo yetu ya chakula na kutimize lengo la kutokomeza hewa ukaa ifikapo mwaka 2050.” 

Guterres pia amesisitiza umuhimu wa usitishaji uhasama wa kimataifa, akisema machafuko na kutokuwepo utulivu ni vichocheo vikubwa vya njaa.  

Amekumbusha ujumbe muhimu wa WFP kwamba “chakula ni amani, na njaa ni jinamizi katika dunia iliyosheheni vitu vingi kikiwemo chakula.” 

Mkutano huu wa kimataifa unajikita katika masuala muhimu na ya haraka yanayohitajika ili kuzuia kuyafanya malengo ya maendeleo endelevu SDGs kuwa ndoto itakayoshindwa kutimia ifikapo mwaka 2030. 

Guterres ameongeza kuwa kufanyakazi kwa ushirikiano, kuondoa vikwazo vya kitaasisi na kushikamana ndiko kutafanya wadau muhimu kutoka Muungano wa Afrika, Umoja wa Mataifa, taasisi za fedha za kimataifa na Muungano wa Ulaya kuweza kutoa rasilimali zinazohitajika kutimiza SDGs na kuzisaidia serikali kutimiza ahadi kwa wananchi wao. 

Naye mkurugenzi mtendaji wa WFP David Beasley katika mkutano huo amesema “Kwa hakika huu ni wakati mgumu usio wa kawaida. Tunakabiliwa na tishio la njaa katika nchi nyingi, huku janga la COVID-19, vita na majanga ya mabadiliko ya tabianchi yakipandisha viwango vya njaa sehemu mbalimbali duniani. Hakuna nchi wala shirika linaloweza kutatua changamoto zote hizi peke yake, tutaweza kuzikabili tu endapo tutashikamana na kufanyakazi pamoja kwa ajili ya mustakabali bora wa dunia nzima.” 

Janga la COVID-19 hadi sasa limeshakatili maisha ya watu zaidi ya milioni 1.3 kote duniani na idadi inaendelea kuongezeka, huku mabadiliko ya tabianchi na njaa vinatishia kuongeza idadi ya vifo duniani. Wadau wa mkutano huo wamesema yote hayo yanaweza kukabiliwa kwa ushirikiano na kukusanya rasilimali zinazohitajika.