Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya wazazi kupima watoto wao utapiamlo Niger yazaa matunda 

Shirika la mpango wa chakula duniani na programu yake ya kuzuia utapiamlo kambi ya Oruchinga nchini Uganda
WFP/Hugh Rutherford
Shirika la mpango wa chakula duniani na programu yake ya kuzuia utapiamlo kambi ya Oruchinga nchini Uganda

Mafunzo ya wazazi kupima watoto wao utapiamlo Niger yazaa matunda 

Afya

Wahenga wanasema usimpe mtu samaki bali mfundishe kuvua ilia pate samaki kila wakati, na hivyo ndivyo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Niger limefanya kwa kuwapatia wazazi ujuzi wa kupimia watoto wao utapiamlo nyumbani badala ya kusubiri kwenda vituo vya afya kama njia mojawapo ya kutokomeza janga hilo linalokumba takribani watoto 400,000 kila mwaka.  

Miongoni mwa familia zinazopata msaada huo ni ile ya Habisatou, mama mwenye umri wa miaka 27 mwenye watoto wawili. 

Habisatou anasema “nilijaliwa watoto watatu, lakini ni wawili tu wako hai. mmoja amefariki dunia.” 

Mtoto wake aitwaye Abou anaugua utapiamlo, na ndio maana ili UNICEF kwa kushirikiana na shirika la kiraia la ALIMA wamechukua hatua ya kuwapatia wazazi ujuzi wa kupima watoto wao ili watambue wana utapiamlo au la. 

Kila mzazi amepatiwa kipima mzingo wa mkono wa mtoto na kuelimisha jinsi ya kuchukua vipimo. 

Habisatou anasema, “nilikuwepo nyumbani pindi mhudumu wa afya wa jamii alipofika nyumbani na kunialika nishiriki mafunzo chini ya mti. “ 

Wakati wa mafunzo hayo mhudumu aliwaelekeza jinsi ya kukifunga kwenye mkono wa mtoto, na iwapo rangi ni nyekundu basi utapiamlo ni wa hali ya juu. 

Habisatou anasema, “sikwenda shuleni, sijui kusoma wala kuandika. Lakini natambua rangi. Tunapopima mkono wa mtoto, na kipimo kikiwa kwenye rangi nyekundu, mtoto ana utapiamlo uliokithiri. Siku mbili baadaye nilimpima mwanangu kwa kuwa niliona anapungua uzito. Na kipimo kikawa rangi nyekundu. Niliogopa mno.” 

Wazazi wanaobaini kuwa watoto wao wana utapiamlo, wanahamasishwa kufika kwenye vituo vya afya wanakopatiwa matibabu na ushauri, pamoja na kubadilishana mawazo kupitia vikundi vya usaidizi vya wazazi.  

Kupitia vikundi hivyo, Habisatou anasema, “tumeoneshwa jinsi ya kulea vema watoto wetu kiusafi, na kuwapatia vyakula sahihi. Nashukuru Mungu sasa ana nafuu, ameanza tena kutambaa na anacheza.”