Ugonjwa wa kisukari wazidi kutesa nchi za kipato cha chini na kati

14 Novemba 2020

Licha ya juhudi za kuzuia na kutibu ugonjwa wa kisukari, bado idadi ya watu wanaougua ugonjwa huo inaongezeka kila uchao.

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres aliyotoa leo kupitia ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya kupambana na ugonjwa wa kisukari.

Amesema kinachotia hofu zaidi, ongezeko la wagonjwa ni katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambazo hazina vifaa vya kutosha vya uchunguzi wa ugonjwa huo, sambamba na dawa za kutibu na uelewa miongoni mwa wananchi ni mdogo.

"Ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona au COVID-19 nao umefanya hali kuwa mbaya zaidi. Bila shaka, wagonjwa wengi wa kisukari hawawezi kupata huduma ya mara kwa mara na matibabu wanayohitaji. Halikadhalika watu wenye kisukari wako hatarini zaidi kuwa na hali mbaya zaidi na kufariki dunia kutokana na COVID-19," amesema Katibu Mkuu.

Mfanyakazi wa huduma za kibinadamu akimsaidia mkimbizi wa Syria mwenye ulemavu ambaye mguu wake ulikatwa kutokana na ugonjwa wa kisukari. Hapa walikuwa wanavuka eneo lililopo kati ya Macedonia na Serbia
Jodi Hilton/IRIN
Mfanyakazi wa huduma za kibinadamu akimsaidia mkimbizi wa Syria mwenye ulemavu ambaye mguu wake ulikatwa kutokana na ugonjwa wa kisukari. Hapa walikuwa wanavuka eneo lililopo kati ya Macedonia na Serbia

Amekumbusha kuwa mwaka ujao wa 2021, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, litazindua mkataba wa kimataifa dhidi ya Kisukari, ambao ni mpango mpya wa kusaidia kuweka muundo wa pamoja wa kupunguza mzigo utokanao na ugonjwa huo.

Ni kwa mantiki hiyo, ametaka ushirikiano zaidi kupitia mpango huo tarajiwa, ili kuhakiisha kuwa "punde tunaweza kupunguza mzigo wa tatizo hili kwenye afya ya umma. Tunapohaha kukabiliana na janga hili, lazima sote tufanye kila tuwezalo kufanikisha huduma ya afya kwa wote, tuimarishe mifumo ya afya na tusongeshe afya na mnepo kwa wote."

Siku ya Kisukari Duniani

Mwaka 2007, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio namba 61/225 likitangaza kuwa tarehe 14 mwezi Novemba kila mwaka iwe siku ya kisukari duniani. Azimio hilo lilitambua udharura wa kusongesha juhudi za kimataifa ili kuendeleza na kuboresha afya ya binadamu, kuhakikisha anapata huduma bora za afya na malezi dhidi ya ugonjwa wa Kisukari.

 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter