Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana tuache kusita, tuache kuwa vuguvugu, tumfuate Anangisye- Getrude

Kitabu kilichoandikwa na msichana Getrude kutoka Tanzania kikilena wasichana kuhusu usawa wa kijinsia.
UN Tanzania/Ahimidiwe Olotu
Kitabu kilichoandikwa na msichana Getrude kutoka Tanzania kikilena wasichana kuhusu usawa wa kijinsia.

Wasichana tuache kusita, tuache kuwa vuguvugu, tumfuate Anangisye- Getrude

Utamaduni na Elimu

Kutana na msichana mtanzania Getrude Mligo, mwanaharakati kijana wa masuala ya kijinsia ambaye mazingira chanya ya makuzi yake yamemjenga na kuweza kuchukua hatua ya kusaidia watoto wengine wa kike na wasichana kujitambua.

Getrude ambaye pia ni mwandishi wa vitabu aina ya riwaya amezungumza na Ahimidiwe Olotu akisema kuwa vitabu vyake ikiwemo kile alichoandika hivi karibuni kwa lugha ya kiingereza, Dear Girl Child vinalenga kufikia usawa wa jinsia na kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. 

Alipoulizwa ni jambo gani lilimsukuma hadi kuandika riwaya inayolenga SDGs, Getrude amesema ni usawa na usuli wa maisha yake. 

“Nimelelewa katika familia ambayo unyanyasaji wa kijinsia haukupatiwa nafasi, hususan kwa baba yangu kwa kuwa nakumbuka kuna kipindi mama yangu alikuwa anatakiwa kwenda masomo nje ya nchi. Mimi nilikuwa na umri mdogo sana wa miezi 9 na nilikuwa nahitaji kunyonya maziwa ya mama. Watu walikuwa wanamshauri baba asiruhusu mwanamke asisafiri nje ya nchi,” amesema Getrude akiongeza watu hao walisema “aende kusoma afanye nini na nani atamlea mtoto ndio wajibu wa mwanamke.” 

Hata hivyo baba mzazi wa Getrude hakuwasikiliza, ingawa ilikuwa ni vigumu kwake kwa kuwa ilibidi aende kazini na huku ahakikishe maendeleo ya mtoto, lakini alimwacha mke wake aende masomoni. 

Getrude anasema suala la jinsia, baba yao hakuwa anazungumza kwa maneno bali alionesha kwa vitendo namna usawa unaweza kuleta maendeleo katika familia. 

“Nasema hivyo kwa sababu kipindi hiki baba yangu ni mgonjwa sana, na mtu pekee ambaye anafanya kazi ni mama yangu na ndiye anamlea baba. Kwa hiyo ina maana kama baba asingemruhusu mama aende masomoni, kipindi hiki alikuwa katika wakati mgumu,” amesema Getrude. 

Akizungumzia safari yake ya uandishi wa vitabu, Getrude anasema alianza mwaka 2017 akiwa mwaka wa kwanza wa chuo. Lakini kabla ya kuanza uandishi, kuna watu waliokuwa wanampa ushauri huku wengine ambao wamemzidi umri wakimkatisha tamaa wakisema kuwa una umri wa miaka 20 kwa nini asisubiri. 

Hata hivyo anasema yeye hakusita bali aliamua kuandika ili aone kile anachotaka kufanya kitafikia wapi. 

Kitabu kinaitwa Dear Girl Child, na amemtumia Anangisye kama msichana anayefikisha ujumbe wa wale wanaopitia ukatili wa kijinsia. 

Alipoulizwa kwa nini Anangisye, Getrude anasema msichana huyo aliamua kuwa wa kitofauti kwa sababu siyo tu jamii ilikuwa inampatia upendeleo, bali kwa sababu alishindwa kusita. 

“Wasichana wengi tunasita na ndio maana nilimchagua Anangisye. Sisi wasichana tunaweza kuwa tunatamani kufanya kitu. Tunafahamu kuwa hiki ni hapana na hiki ni ndio, lakini nasita kufanya uamuzi, nakuwa katikati. Hiki kitabu kinamtaka msichana asigande, asiwe kama amegandishwa kwenye barafu,” amesema Getrude. 

Kitabu hicho alichoandika kwa lugha ya kiingereza kimeandaliwa kwa ushirikiano na Msichana Initiative, Higher Initiative, Bright Jamii na Hope for Young Girls  kwa lengo la kuhakikisha kitabu kinasambazwa na kufikia wasichana wengi zaidi. 

Hivi sasa nakala 700 za kitabu hicho zimesambazwa shuleni na mipango imekamilika ili kiweze kupatikana kwa mtandao.