Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO/UNICEF kutoa chanjo dhidi ya polio kwa kwa Watoto milioni 1.5 Sudan Kusini

Mtoto mchanga akipewa chanjo dhidi ya polio Juba, nchini Sudan Kusini mnamo Machi 2020.
© UNICEF/Helene Sandbu Ryeng
Mtoto mchanga akipewa chanjo dhidi ya polio Juba, nchini Sudan Kusini mnamo Machi 2020.

WHO/UNICEF kutoa chanjo dhidi ya polio kwa kwa Watoto milioni 1.5 Sudan Kusini

Afya

Kampeni kubwa ya chanjo imezinduliwa leo nchini Sudan Kusini na mashirika ya Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO na la kuhudumia Watoto UNICEF kwa lengo la kuwachanja watoto milioni 1.5 dhidi ya polio baada ya mlipuko mpya kusababisha kupooza kwa watoto 15.

Kwa mujibu wa mashirika hayo hivi sasa kuna wagonjwa 15 wa polio waliothibitishwa katika kaunti 15 kwenye majimbo matano ya nchi hiyo ambayo ni Bahr El Ghazal Kaskazini, Bahr El Ghazal Magharibi, Warrap, Lakes na Equatoria Mashariki. 

Visa hivyo vimeelezwa kuwa miongoni mwa watoto wa chini ya umri wa miaka mitano na wamepata ugonjwa wa kupooza ambao hauwezi kutibika. 

Ili kuzuia kusambaa kwa mlipuko huo wa polio wizara ya afya ya Sudan Kusini imeunda kikosi kazi cha dharura kinachojumuisha WHO, UNICEF na wadau wengine ili kuweka mipango ya dharura kukabiliana na mlipuko huo wa polio huku ikiongeza juhudi za ufuatiuliaji, mikakati ya uzuiaji na mbinu za kuudhibiti. 

WHO na UNICEF wamesema njia pekee ya kukomesha kusambaa na kuzuia watoto wengi kutopata virusi hivyo hatari vya polio ni kupitia chanjo na kampeni hiyo ya chanjo itafanyika katika majimbo sab ana kaunti 45 katika awamu ya kwanza huku mipango ikiendelea kwa ajili ya majimbo mengine. 

Waziri wa afya wa Sudan Kusini Elizabeth Achue amesema“Tunahitaji kuchukua hatua haraka kuzuia mlipuko huu kuathiri watoto wengi zaidi na natoa wito kwa wazazi wote kupeleka Watoto kwenye vituo vya chanjo wakiwemo wale ambao tayari wameshachanjwa, ni salama kupata dozi nyingine ya chanjo kwani tunataka kuhakikisha Watoto wote wanalindwa.” 

Mwakilishi wa WHO Sudan Kusini Dkt. Olushayo Olu amesema “Hakuna mtoto yoyote popote anayepaswa kuugua polio ugonjwa ambao unaweza kuzuilika kwa chanjo. Licha ya janga la COVID-19 linaloendelea na mafuriko, kampeni hii inatoa fursa kwa walio hatarini kupata chanjo muhimu na kuepuka ugonjwa wa kupooza.” 

Naye mwakilishi wa UNICEF nchini humo Mohamed Ayoya amesisitiza kuwa “chanjo ni lazima na kutopata ni kununu kifo. Ni lazima tuhakikishe Watoto wote Sudan Kusini wanapata chanjo muhimu ikiwemo ya polio.” 

Mashirika hayo yamesema nchini Sudan Kusini watoto waliopata chanjo dhidi ya polio na magonjwa mengine yanayotishia Maisha ni chini ya asilimia 50.