Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kifo 1 kati ya 5 vya COVID-19 Afrika kinahusiana na kisukari:WHO 

Mhudumu wa afya akimchunguza mgojwa wa kisukari kiwango cha sukari mwilini
WHO/A. Loke
Mhudumu wa afya akimchunguza mgojwa wa kisukari kiwango cha sukari mwilini

Kifo 1 kati ya 5 vya COVID-19 Afrika kinahusiana na kisukari:WHO 

Afya

Katika kuelekea siku ya kisukari duniani itakayoadhimishwa kesho Novemba 14, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limebaini kwamba kifo kimoja kati ya vitano vya corona au COVID-19 barani Afrika kinahusiana na ugonjwa wa kisukari.

Kwa mujibu wa WHO asilimia 18.3 ya vifo vya COVID-19 vilivyotokea Afrika ni miongoni mwa watu wenye ugonjwa wa kisukari ambao huongeza hatari ya hali mbaya na vifo kwa watu walioambukizwa virusi hivyo. 

Tathimini ya shirika hilo la afya katika nchi 14 za Afrika ambazo zimetoa taarifa kuhusu COVID-19 na matatizo ya kiafya ya muda mrefu, imeonyesha kwamba hatari ya kuugua mahtuti au hata kufa kutokana na COVID-19 miongoni mwa watu wenye kisukari inaongezeka kutokana na umri, huku watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi. 

Kisukari WHO inasema ni chanzo kikubwa cha upofu, figo kushindwa kufanya kazi, kiharusi, shinikizo la damu na kukatwa viungo mwa mwili kama miguu. 

Lakini kwa kupipwa na kupata matibabu ya mapema, athari nyingi za ugonjwa huo zinaweza kucheleweshwa au kuepukwa.  

Dkt. Jean Marie Dangou mratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza NCD's katika ofisi ya WHO Afrika anasema tatizo ni  uelewa finyu kuhusu ugonjwa huo,“Kiwango cha uelewa wa kisukari barani Afrika ni kidogo sana , kuna fursa duni za kubaini mapema na upimaji wa kisukari kwa watu. Mwaka 2018 tuliorodhesha wagonjwa milioni 15.9 wa kisukari na vifo 312,000 vilivyotokana na ugonjwa huo. Hii inaogopesha, na mbali ya hayo watu zaidi ya asilimia 50 wanaoishi na kisukari hawatambui hali yao.” 

Ukanda wa Afrika tathimini hiyo inasema umeshuhudia kisukari kikiongezeka mara sita kutoka wagonjwa milioni 4 mwaka 1980 hadi wagonjwa milioni 25 mwaka 2014 na barani humo asilimia 60 ya watu wanaishi na kisukari bila kujua. 

Mathalani utafiti uliofanyika nchini Kenya uligundua kwamba asilimia 60 ya watu waliokutwa na magonjwa sugu na ya muda mrefu hawakuwa katika matibabu yoyote. 

 Akisistiza umuhimu wa kuzingatia vita dhidi ya kisukari mkurugenzi wa WHO Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesem“ Watu wengi wako gizani linapokuja suala la kutambua kama wana kisukari ama la. Watu wenye magonjwa sugu wanapata pigo mara mbili endapo wataambukizwa COVID-19. Lazima tubadili hali hii kwa kuwekeza katika kugundua mapema, kuzuia na kutibu kisukari, tusipoteze mwelekeo” .

 Ameongeza kuwa ukanda wa Afrika pia unashuhudia ongezeko la hatari za kupata kisukari kama vile utipwatipwa kutokana na kubadili mfumo wa maisha na matumizi ya vyakula vyenye kiwango kikubwa cha sukari, mafuta na chumvi, kiwango ambacho ni kati ya asilimia 2.5 miongoni mwa watu wazima Burundi hadi asilimia 26.9 kwenye visiwa vya Ushelisheli. 

 Hivi sasa WHO inafanyakazi kwa karibu na nchi za Afrika ili kutoa mafunzo wa kwauguzi na wahudumu wengine wa afya na kupanua wigo wa fursa za upimaji, uzuiaji na matibabu ya kisukari. 

 Ugonjwa wa kisukari unatokea wakati ambapo kongosho linashindwa kuzalisha insulin ya kutosha na ndipo mtu anapata kisukari aina ya 1 ama wakati mwili unaposhindwa kutumia insulini uliyozalisha na mtu kupata kisukari aina ya 2 ambayo ndiyo inayowakumba watu wengi duniani.