Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji 74 wafa maji Mediteranea 

Wafanyakazi wa IOM walihusika na shughuli za uokozi wakati boti lilipozama kwenye ufukwe wa Libya.(Maktaba)
IOM/Hussein Ben Mosa
Wafanyakazi wa IOM walihusika na shughuli za uokozi wakati boti lilipozama kwenye ufukwe wa Libya.(Maktaba)

Wahamiaji 74 wafa maji Mediteranea 

Wahamiaji na Wakimbizi

Wahamiaji wapatao 74 wamekufa maji hii leo baada ya boti walimokuwa wakisafiria kuzama kwenye eneo la Khums karibu na pwani ya Libya. 

Shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) linasema janga la leo ni miongoni mwa matukio manane ya kuzama kwa boti kwenye eneo la Mediteranea ya Kati tangu tarehe 1 mwezi Oktoba mwaka huu. 

Taarifa ya IOM iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi hii leo imesema kuwa boti ya leo imeripotiwa kuwa ilikuwa imebeba watu 120, miongoni mwao ni wanawake na watoto. 

“Manusura 47 wameokolewa na  walinzi wa pwani pamoja na wavuvi na kusafirishwa hadi ufukweni huku miili 31 imeopolewa na maiti wengine wanaendelea kutafutwa,” imesema taarifa hiyo. 

Ni watu 47 pekee walionusurika kwenye boti hiyo iliyokuwa imebeba watu zaidi ya 120. Boti imezama karibu na pwani ya Libya leo Alhamisi Novemba 12, 2020.
IOM/Hussein Ben Mosa
Ni watu 47 pekee walionusurika kwenye boti hiyo iliyokuwa imebeba watu zaidi ya 120. Boti imezama karibu na pwani ya Libya leo Alhamisi Novemba 12, 2020.

Katika siku mbili zilizopita, takribani watu 19 wakiwemo watoto wawili, walizama baada ya boti mbili kuzama kwenye eneo hilo la Mediteranea ya Kati, huku meli iitwayo Open Arms, meli pekee ya shirika la kiraia la uokozi inayotoa huduma kwenye njia hiyo, ikiokoa zaidi ya watu 200 katika operesheni tatu. 

Mkuu wa IOM Libya, Federico Soda amesema ongezeko la vifo kwenye bahari ya Mediteranea linatokana na kushindwa kwa nchi kupitisha uamuzi wa kijasiri wa kuweka mfumo thabiti na bora wa kuokoa watu kwenye njia hiyo hatari zaidi ya baharini. 

Bwana Soda amesema, “kwa muda mrefu tumetaka mabadiliko ili kuondoa mfumo wa sasa usiofanya kazi Libya na kwenye bahari ya Mediteranea na kuweka mfumo dhahiri wa kunusuru ambao utaunga mkono na mataifa mengine.” 

Amesema maelfu ya watu wanaendele kulipa gharama ya kushindwa kuchukuliwa kwa hatua thabiti iwe baharini au nchi kavu. 

Mwaka huu pekee, takribani watu 900 wamekufa maji kwenye bahari ya Mediteranea wakijaribu kuvuka kuelekea pwani za Ulaya, na vifo vyao vinatokana na kuchelewa kuokolewa. 

Watu wengine zaidi ya 11,000 wamerejeshwa Libya na kuwaweka hatarini zaidi kukumbana na ukiukwaji wa haki za binadamu, kuwekwa korokoroni, kunyanyaswa au kusafirishwa kiharamu.