Bado wakulima wadogo wadogo waambulia fedha kidogo za kujenga mnepo dhidi ya tabianchi- Ripoti 

12 Novemba 2020

Ripoti mpya iliyotolewa leo kuhusu ufadhili wa fedha kwa wakulima wadogo wadogo wanaokumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika nchi zinazoendelea imebaini kuwa licha ya kiwango kikubwa cha fedha kuchangishwa kuwasaidia bado wakulima hao wanaambulia kiwango kidogo cha fedha kuweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD na mpango wa kisera kwa tabianchi, CPI wametoa ripoti hiyo wakisema kuwa ni asilimia 1.7 ya fedha huelekezwa kwa wakulima hao licha ya kwamba wao ndio wako hatarini zaidi kukumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. 

Ripoti inataja viwango vya juu vya joto, ukame, mafuriko husambaratisha mazao na mifugo na kusababisha wakulima katika mashamba madogo milioni 500 duniani kote washindwe kulisha familia zao na pia kupata kipato. 

Ripoti hiyo inaenda mbali zaidi ikieleza kuwa kwa kuwa wakulima hao ndio wanazalisha asilimia 50 ya chakula duniani, basi hali ya njaa inaweza kuongezeka iwapo watashindwa kuendelea na uzalishaji. 

Grace Mukamana, mkulima wa mahindi kutoka Rwanda ni shuhuda. 

Grace anasema, “kwa kweli haya mabadiliko ya hali ya hewa yananitisha mno. Jua ni kali mno na mawingu hayatulii.” 

Ikiwa imepatiwa jina Uchunguzi wa pengo la ufadhili wa fedha kwa wakulima wadogo wadogo, ripoti hiyo imebaini kuwa ufadhili wa miradi ya kujenga mnepo kwenye mabadiliko ya tabianchi ulivuka dola nusu trilioni kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na 2018 lakini wakulima wadogo wadogo waliambulia dola milioni 10 pekee. 

Ni kwa mantiki hiyo IFAD inataka uwekezaji zaidi kwa wakulima hao walio hatarini, ikisema fedha zaidi siyo tu zitawanufaisha wakulima hao bali pia jamii nzima ya kimataifa. 

Marguerita Astalaga, ni Mkurugenzi wa IFAD akihusika na masuala ya mazingira, tabianchi na ujumuishwaji wa kijamii na anasema, “Ufadhili wa miradi ya tabianchi unaoelekezwa kwa wakulima wadogo huwezesha kuendelezwa kwa uzalishaij wa chakula bora, nafuu na chenye lishe kwa jamii kubwa zaidi. Hii ina maana kuwa uwekezaji huu unasaidia kutokomeza njaa, ni uwekezaji kwa amani duniani, ustawi na utulivu.” 

Mradi wa IFAD wa kujenga mnepo kwa wakulima wadogo, ASAP, ni moja ya miradi mikubwa zaidi duniani inayolenga wakulima

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter