Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nosizi Reuben, mshona wa kwanza mwanamke Kenya kuingia Chuo Kikuu 

Mwanamke, ambaye wazazi wake wanatokea Zimbabwe amekuwa mtu wa kwanza asiyekuwa na utaifa kwenda chuo kikuu nchini Kenya.
© UNHCR/Anthony Karumba
Mwanamke, ambaye wazazi wake wanatokea Zimbabwe amekuwa mtu wa kwanza asiyekuwa na utaifa kwenda chuo kikuu nchini Kenya.

Nosizi Reuben, mshona wa kwanza mwanamke Kenya kuingia Chuo Kikuu 

Utamaduni na Elimu

Nchini Kenya ndoto ya masomo ya elimu ya juu ya Nosizi Reuben ambaye ni mzaliwa wa wazazi wa kabila la washona waliowasili nchini humo kutoka iliyokuwa Rhodesia sasa Zimbabwe miaka ya 1960 sasa imeanza kutimia baada ya kupatiwa cheti cha kuzaliwa.

Nosizi Reuben mwenye umri wa miaka 20 ni mtoto wa 4 katika familia ya watoto wanane, ambao kwa kawaida wasichana huolewa mapema kwa kuwa hakuna matarajio ya kujiendeleza kimasomo kutokana na kukosa vyeti vya kuzaliwa. 

Wazazi wa Nosizi waliwasili Kenya miaka ya 1960 wakieneza dini wakiwa na hati za kusafiria za iliyokuwa Rhodesia na walisajiliwa kama vijakazi wa waingereza. 

Baada  ya uhuru wa Kenya mwaka 1963 hawakuwa na kitambulisho cha utaifa na hivyo walisalia bila utaifa wakikosa huduma za msingi kama vile elimu na bima ya afya na hata hawakuweza kusafiri au kumiliki mali. 

Hali hii ilimuweka Nosizi katika mazingira magumu kwani licha ya kufanya vizuri darasani, fursa za kuendelea elimu ya juu zilizidi kuwa finyu. 

Hata hivyo mama yake amekuwa akitumia tangazo la uzazi kuomba akubaliwe kuendelea na masomo ya sekondari ya juu na hatimaye mwaka jana kufuatia juhudi za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na Kamisheni ya haki za binadamu Kenya, KHCR, watoto wa kishona walipatiwa vyeti vya kuzaliwa. Nosizi naye alipatiwa cheti ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kumaliza sekndari ya juu. 

Nosizi alifaulu mtihani wa kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya na sasa yuko mwaka wa kwanza akisomea shahada ya Uchumi huku akiwa mwanamke wa kwanza wa kishona kufikia hatua hiyo. 

“Nilipogundua najiunga na Chuo Kikuu, ilikuwa ni jambo zuri zaidi katika maisha yangu. Nikiwa ni msichana nisiye na utaifa, imekuwa ni safari yenye changamoto nyingi lakini nzuri kuweza kufika hapa nilipo,” amesema Nosizi huku akiongeza kuwa sasa amekuwa chanzo cha motisha kwa wadogo zake. 

Sasa Nosizi anataka kuwa mfano kwa watoto wengine wa kike wa kabila la kishona, akisema, nataka wasichana wa kishona waone kuwa wanaweza kuwa chochote kile watakacho. Nataka kuwa mfano kwa wadogo zangu wa kike. Nataka nivunje mwiko ya kwamba wasichana wa kishona lazima waolewe wakiwa wadogo.” 

Nchini Kenya inakadiriwa kuna watu 18,000 wasio na utaifa wakiwemo wale wenye asili ya Zimbabwe na Msumbiji pamoja na Burundi, DR Congo, India na Rwanda.