Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumechoka tunataka kurejea nyumbani wakimbizi Nigeria wamwambia Amina J. Mohammed 

Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed alipokutana na msichana katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria
United Nations/Daniel Getachew
Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed alipokutana na msichana katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria

Tumechoka tunataka kurejea nyumbani wakimbizi Nigeria wamwambia Amina J. Mohammed 

Amani na Usalama

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yuko ziarani Afrika Magharibi na ukanda wa sahel na jana Jumanne alizuru jimbo la Borno Kaskazini Mashariki mwa Nigeria. 

Jimbo hilo limeathirika vibaya na vita na watu wengi wanaendelea kuishi chini ya vitisho vya uasi wa kundi la kigaidi la Boko Haram. 

Akiwa mjini Banki karibu na mpaka wa Nigeria na Cameroon , Naibu Katibu Mkuu Amina J. Mohammed alitembelea kambi inayohifadhi wakimbizi wa ndani pamoja na wakimbizi wa Nigeria wanaorejea nyumbani kutoka Cameroon. 

Ziara hiyo katika mji wa mpakani ilikuwa ni ya kujionea ushirikiano baina ya jimbo hilo, serikali na Umoja wa Mataifa na msaada wake kwa jamii zilizotawanywa na jinsi gani ushirikiano huo unavyoendelea amesema Bi. Mohammed. 

Ameongeza kuwa “Tuliweza kuwatembelea wakimbizi wengi wa ndani na kwa hakika maelfu tuliowakuta katika kambi hiyo wanataka kwenda nyumbani, na wamechoka kuvumilia hilo. Wanapenda kurejea katika Maisha yao, kuweza kupata tena fursa ya huduma za msingi na hilo nadhani lilikuwa bayana katika ziara yetu ya leo.” 

Bi. Mohammed pia amezungumzia msaada unaotolewa na kambi hiyo kwa watu waliotawanywa pamoja na wale wanaorejea na “kutafuta njia ya kuwapa makazi mapya na kuwajumuisha watu wa Borno katika Maisha ya amani na mfanikio, yaliyo bora kuliko walipoondoka ambapo wamekuwa wakipitia miaka mingi ya vita.” 

Amesema ameridhishwa kuona kwamba kituo cha mpakani mjini Banki kinatoa fursa ya hali ya kiraia na matumaini ni kwamba kitaanza kurejesha hali ya kawaida mjini hapo ingawa itachukua muda kwa Maisha kurejea kikamilifu katika hali ya kawaida. 

Mbali ya changamoto zinazohusiana na usalama na mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka , Naibu Katibu Mkuu amejionea juhudi zinazochukuliwa na serikali , mashirika yasiyo ya kiserikali au NGO’s na wadau wengine katika kukabiliana na athari za janga la corona au COVID-19 katika baadhi ya jamii zilizo hatarini zaidi katika taifa hilo. 

Baadaye siku hiyo Bi.Mohammed alisfiri kwenda Maiduguri ambako alikutana na gavana wa jimbo la Borno. Pia alitembelea shule ya sekondari ya wasichana na kufanya mazungumzo na wahudumu wa masuala ya kibinadamu. 

Naibu Katibu Mkuu yuko katika ziara ya mshikamano ya wiki mbili Afrika Magharibi na Sahel kwenda kusisitiza uungaji mkono wa umoja wa Mataifa katika nchi hizo wakati huu wa janga la COVID-19. 

Alianza ziara yake Jumatatu nchini Nigeria ambako alikutana na Rais Muhammadu Buhari na maafisa wengine wa ngazi ya juu mjini Abuja.