Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maandalizi ya MINUSCA na vikosi vya usalama CAR kwa ajili ya uchaguzi yashika kasi 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ukiweka ulinzi kwenye makao makuu ya kusimamia uchaguzi.
MINUSCA/Francis Yanbedji
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya kati ukiweka ulinzi kwenye makao makuu ya kusimamia uchaguzi.

Maandalizi ya MINUSCA na vikosi vya usalama CAR kwa ajili ya uchaguzi yashika kasi 

Amani na Usalama

Polisi wa Umoja wa Mataifa UNPOL walioko katika mpango wa kuweka utulivu nchini Janhuri ya Afrika ya Kati ujulikanao kama MINUSCA wanafanya maandalizi ya pamoja na vikosi vya  usalama vya CAR ili kuhakikisha wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa Desemba mwaka huu mambo yanakuwa shwari.

Katika mitaa ya mji mkuu Bangui hali ni ya tafran huku vikosi vya usalama vya serikali na polisi wa Umoja wa Mataifa wakijaribu kuikabili. Na kinachoendelea sio mashambulizi wala machafuko halisi bali ni mazoezi ya mfano ya kujiandaa endapo vurugu na machafuko yatazuka wakati wa uchaguzi wa tarehe 27 Desemba mwaka huu nchini humo. 

Mazoezi haya ya mfano yaliyofanyika mjini Bangui na viunga vyake yanayojumuisha uwezekano wa matukio mbalimbali, yanaendeshwa na mpango wa MINUSCA ambao mkuu wake Mankeur Ndiaye anasema,“Mazoezi haya ni muhimu sana kwa sababu tunakaribia tarehe ya uchaguzi, kutakuwa na maandamano mengi, maandamano ya kijamii na ya kisiasa. Na chochote kinawezekana, tuko katika nchi iliyoghubikwa na vita.” 

Mazingira ya matukio mbalimbali yametumika kuandaa mazoezi haya kama vile kushambuliwa kwa mji wa Bangui na makundi yenye silaha kutoka kwenye majimbo au kwa waasi maarufu. Bwana Ndiaye anasema ni bora kujiandaa kuliko kushtukizwa, “Changamoto nyingi zinatusubiri, na mazoezi haya yanakwenda sanjari na mtazamo huo. Tutawezaje kukidhi changamoto za usalama wakati tunajua kwamba lengo letu ni kuulinda umma?. Hatuko hapa kukandamiza waandamanaji, tuko hapa kwa ajili ya kutekeleza uhuru wa demokrasia na uhuru wote, lakini kwa kuheshimu sheria.” 

MINUSCA inasema mazoezi haya ya ushirikiano na jeshi la CAR na vikosi vya usalama ni ya kuhakikisha kwamba uchaguzi ujao unafanyika kwa usalama.