Skip to main content

COVID-19 yaathiri wahamiaji na utumaji fedha nyumbani 

COVID-19 inasababisha njaa kubwa, mfanyakazi wa WFP akizungumza na watu katika kambi ya wakimbizi wa ndani.
WFP/Oluwaseun Oluwamuyiwa
COVID-19 inasababisha njaa kubwa, mfanyakazi wa WFP akizungumza na watu katika kambi ya wakimbizi wa ndani.

COVID-19 yaathiri wahamiaji na utumaji fedha nyumbani 

Wahamiaji na Wakimbizi

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imebaini kuwa viwango vya  njaa na ukimbizi ambavyo tayari vilikuwa vimevunja rekodi kabla ya mlipuko wa wa ugonjwa wa Corona au COVID-19,  vitazidi kuongezeka wakati huu ambapo wahamiaji na wategemezi wa fedha kutoka nje wanahaha kusaka kazi ili kusaidia familia zao. 

Ripoti hiyo ya kwanza ya aina yake imetolewa leo huko Roma Italia na Geneva Uswisi, na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la uhamiaji, IOM na lile la mpango wa chakula duniani, WFP. 

Mathalani inaonesha jinsi janga la Corona limeongeza ukosefu wa chakula na kuwaweka hatarini zaidi wahamiaji, walio kwenye mizozo na majanga pamoja na familia zinazotegemea upokeaji wa fedha kutoka kwa jamaa. 

  Mashirika hayo yameonya kuwa madhara ya kiuchumi na kijamii kutokana na janga la Corona yanaweza kuwa makubwa na hivyo kutoa wito kwa dunia kuchukua hatua haraka ili kukidhi mahitaji ya kibinadamu yanayoongezeka na kushughulikia athari za kiuchumi na kijamii bila kusahau wale walio hataraini zaidi. 

  Mkurugenzi Mtendaji wa WFP David Beasley amesema madhara ya  kiuchumi na kijamii yasababishwayo na COVID-19 yanatisha kuliko hata janga lenyewe. 

“Watu wengu katika nchi za kipato cha chini na kati ambao miezi michache iliyopita walikuwa masikini lakini waliweza kumudu maisha, sasa wanaona kabisa maisha yao yamesambaratishwa. Fedha walizokuwa wanapokea kutoka kwa wafanyakazi walio nje ya nchi zimekauka na kusababisha hali ngumu mno. Matokeo yake, viwango vya njaa vimeongezeka duniani kote,” amesema Beasley. 

  Naye Antonio Vitorino ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa IOM amesema athari za COVID-19 katika afya na mienendo ya uhamiaji ya binadamu, vinatishia kurudisha nyuma ahadi za kimataifa ikiwemo mkataba wa kimataifa kuhusu uhamiaji na usaidizi kwa wale wenye uhitaji. 

“Ni wajibu wetu wa pamoja kulinda haki za watu wanaohamahama na kuhakikisha tunawaepusha na madhara zaidi,” amesema Vitorino. 

  Ripoti inafafanua kuwa vikwazo vya kutembea ili kuepusha kusambaa kwa COVID-19 katika nchi zaidi ya 220 vimeathiri mno wahamiaji na wakimbizi wa ndani, hasa kwa kubinya fursa za ajira zinazowawezesha kupata kipato na hivyo kushindwa kupata mlo na hata kutuma fedha kwa wapendwa wao kule walikowaacha. 

  Hali ni mbaya zaidi kwani idadi kubwa ya wakimbizi na wahamaiji iko katika nchi ambazo tayari zina ukosefu wa chakula na pia zinakabiliwa na utapiamlo. 

Takwimu zinaonesha kuwa wahamimiaji wafanyakazi milioni 164 hususan wale wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi, ni miongoni mwa walioathiriwa zaidi na COVID-19. 

Mara nyingi wanafanya kazi za vibarua, ujira ukiwa mdogo na bila kuwa na uhakika wa hifadhi ya jamii kama vile pensheni na wakati wa janga la kiuchumi wao ndio wa kwanza kupoteza ajira. 

Ripoti inasema kuwa bila kipato endelevu, wahamiaji wengi siyo tu watalazimika kurejea nyumbani bali pia kiwango cha utumaji fedha nyumbani kitaporomoka, wakati fedha hizo ni tegemeo kwa watu milioni 800 duniani kote, saw ana mtu mmoja kati ya 9.