Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la afya duniani lafungua pazia kwa wito wa kuachana na ubinafsi-WHA 

Sehemu ya kujivinjari jijini New York ambapo michoro imewekwa kuhakikisha watu wanazingatia umbali unaofaa kwa ajili ya COVID-19.
UN News/Daniel Dickinson
Sehemu ya kujivinjari jijini New York ambapo michoro imewekwa kuhakikisha watu wanazingatia umbali unaofaa kwa ajili ya COVID-19.

Baraza la afya duniani lafungua pazia kwa wito wa kuachana na ubinafsi-WHA 

Afya

Mkurugenzi mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amewaambia nchi wanachama wa shirika hilo kwamba juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na umasikini zimepata pigo kwa sababu ya kukosekana kwa umoja wa kimataifa tangu kupitishwa wa maafikiano ya kimataifa ya malengo ya maendeleo endelevu SDG’s miaka mitano iliyopita na pia amekaribisha fursa ya kufanyakazi na serikali mpya ya Marekani inayotarajiwa ya Rais mteule Joe Biden. 

Akizungumza hii leo mjini Geneva Uswis katika ufunguzi wa kuanza kwa baraza la afya duniani WHA, baada ya mkutano huo wa kila mwaka kukatishwa mwezi Mei mwaka huu kutokana na janga la corona au COVID-19, Dkt. Tedros amesema dunia ilifanikiwa kushikamana mwaka 2015 wakati serikali zilipopitisha malengo ya maendfeleo endelevu, mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris na ajenda ya kuchukua hatua ya Addis Ababa kuhusu ufadhili kwa ajili ya maendeleo. 

Lakini amesema “Tangu wakati huo wimbi la kusambaa kwa utaifa uliopotoka na kujitenga kumedhoofisha hali ya kusudi la Pamoja. Mkataba wa Paris umedhoofishwa, ahadi zilizotolewa katika ajenda ya addis Ababa yah atua hazijatimizwa kabisa na ingawa kumekuwa nah atua kuelekea SDG’s mara nyingi juhudi zetu zimesalia kuwa binafsi na zilizogawanyika”. 

Ameongeza kuwa janga la COVID-19 limerudisha nyuma ahata zaidi juhudi za kufikia SDG’s ingawa pia limedhihirisha umuhimu wake. 

Lengo la pamoja 

Dkt. Tedros amesisitiza kwamba “Hata hivyo ni lazima tuwe wawazi,tunaweza tu kutambua na nguvu na uwezekano wa SDG’s endapo jumuiya ya kimataifa itafanya haraka kurejea kwenye dhamira ya pamoja ambayo ndiyo iliyozaa malengo hayo . Na kwa ari hiyo tunampongeza Rais mteuule wa Marekani Joe Biden na makamu wa Rais mteule Kamala Harris na tunatarajia kushirikiana na uongozi wao kwa karibu.” 

Ameongeza kuwa umewadia wakati wa zama mpya za ushirikiano zenye kutilia mkazo afya na ustawi wa dunia nzima. 

“Huu ni wakati wa dunia kupona kutoka kwenye zahma za janga la COVID-19 na migawanyiko ya kijiografia na kisiasa ambayo inatusukuma sote kutumbukia katika mustakabali usio na afya, usio salama na usio na usawa.” 

Dunia imefika njiapanda 

Mkuu huyo wa WHO amesisitiza kwamba “Dunia imefika pabaya njiapanda. Hatuwezi kuendelea kuisukuma hewa ukaa katika anga zetu katika kiwango kilekile na kuweza kuvuta hewa safi. Ni lazima tuchague. Hatuwezi kumudu ongezeko Zaidi la pengo la usawa na kutarajia amani na mafanikio viendelee, ni lazima tuchague. Na hatuwezi kumudu kuona afya inachukuliwa kama kitu cha maendeleo au bidhaa ambayo ni matajiri tu wanaoweza kumudu. Leo na kila siku tunapaswa kuchagua afya, sisi ni familia moja kubwa.”