Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimbunga Eta kimepita Nicaragua, lakini athari zake zitabaki kwa muda:UNICEF 

Bibi akiwa na mjukuu wake katika kitongoji cha El Muelle kwenye mji wa Puerto Cabezas nchini  Nicaragua ambako kimbunga ETA kimeleta madhara makubwa.
UNICEF/Tadeo Gómez
Bibi akiwa na mjukuu wake katika kitongoji cha El Muelle kwenye mji wa Puerto Cabezas nchini Nicaragua ambako kimbunga ETA kimeleta madhara makubwa.

Kimbunga Eta kimepita Nicaragua, lakini athari zake zitabaki kwa muda:UNICEF 

Msaada wa Kibinadamu

Kimbunga Eta kilicholikumba eneo la Amerika ya Kati katika juma zima lililopita sasa kimepita lakini kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF athari zake hususan nchini Nicaragua zitasalia kwa muda mrefu.

Katika makazi ya El Muelle jimbo la Bilwi nchini Nicaragua uharibifu uliosababishwa na kimbunga Eta ni dhahiri, kuanzia miundombinu kama barabara, shule, vituo vya afya na makazi ya watu kwenye mji huu ulioko pwani. 

Kimbunga hicho kilikuwa na kasi ya kiwango cha daraja la 4 na kiliambatana na mvua kubwa upepo mkali, mafuriko na maporomoko ya udongo. Watu zaidi ya milioni moja na laki mbili wameaathirika Nicaragua wakiwemo watoto karibu 500,000. 

Mayadana Servantes mwenye umri wa miaka 24 ni mama anayelea watoto wake wawili peke yake katika makazi ya El Muelle, amepoteza kila kitu ikiwemo nyumba yake kutokana na kimbunga hiki na anasema “Kimbunga hiki kimesambaratisha kabisa maisha na nyumba yangu, sina chochote, hata maji ya kunywa, nguo au godoro. Hatuna kitu chochote cha kulalia. Kwa kuwa ninaishi karibu na ufukweni na nina watoto wawili nikasema hatuwezi kukaa hapa, kulikuwa na maji mengi sana na yakafika na kusomba nyumba yangu. “ 

Watoto kwenye kitongoji cha El Muelle huko Puerto Cabazes nchini Nicaragua ambako kimbunga ETA kimesababisha madhara makubwa.
UNICEF/Tadeo Gómez
Watoto kwenye kitongoji cha El Muelle huko Puerto Cabazes nchini Nicaragua ambako kimbunga ETA kimesababisha madhara makubwa.

UNICEF na washirika wake nchini Nicaragua waliweka mpango maalum na sasa wameanza kusambaza misaada ya dharura ili kushughulikia mahitaji ya haraka na ya lazima kwa watoto na familia zao wakiwemo watu 10,000 waliohamishwa kutoka eneo la Cayos Miskitos na maeneo mengine yaliyoathirika vibaya ya kimbunga hicho kwenye pwani ya kaskazini ya nchi hiyo. Kwa Mayadana kikubwa zaidi ni kwamba ,“Sina nyumba, na tuko peke yetu, ni mimi tu na watoto wangu wawili, hatuna nguo, vyombo vya kupikia na tumebaki watupu bila chochote, hata godoro tu hatuna.” 

Kwa mujibu wa Paolo Sassaro naibu mwakilishi wa UNICEF nchini Nicaragua miongoni mwa msaada wanaotoa kwa waathirika hawa ni pamoja na vifaa vya kujisafi, madumu ya maji, tembe za kusafisha maji na vifaa vya kupima ubora wa maji, msaada ambao utakidhi mahitaji ya dharura ya watu 15,000 wakiwemo watoto 6,000.  

Pamoja na msaada huo UNICEF inasema uharibifu ni mkubwa na athari zake zitaendelea kwa muda mrefu wakati waathirika wakisaka njia za kujenga upya maisha yao.